Kenya: Washika dau wa sekta ya utalii watarajia idadi ya watalii kuongezeka
2021-07-20 08:01:12| CRI

Wadau katika sekta ya utalii nchini Kenya wana imani kuwa watalii wa kigeni wataongezeka nchini miezi ijayo. Hii inafuatia ripoti iliyotolewa na wizara ya utalii wiki iliyopita, ikionyesha kuwa Kenya ilipokea watalii 305,635 kati ya mwezi Januari na Juni mwaka huu. Kati ya hao, 96,003 walikuwa wa kike, na 209,632 walikuwa wa kiume.

Kenya ilipokea watalii wengi kutoka Marekani, ambao walikuwa 49,178, watalii kutoka Uganda walikuwa 31,418, Tanzania 31,291, China 18,069, Uingereza 16,264, India 13,950, na watalii kutoka Rwanda walikuwa 9,800.

Sekta ya utalii bado imeathirika haswa eneo la Pwani, kwani kuna baadhi ya hoteli za ufuoni bado hazijafunguliwa.

Hata hivyo, kufuatia jitihada za serikali kuu pamoja na serikali za kaunti za kutangaza utalii wa Kenya, idadi ya watalii wa ndani nan je inazidi kuongezeka, hii ikiwa ni ishara nzuri kwa sekta hii.