Wakulima Kiambu Wapokea Hundi Ya Sh39 Milioni Kupiga Jeki Shughuli Zao Za Kilimo
2021-08-11 07:51:23| CRI

SERIKALI ya Kaunti ya Kiambu imetoa hundi ya Sh39 milioni kwa wakulima ili waimarishe shughuli zao za kilimo.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, amesema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kuwapa wakulima hao mwelekeo wa jinsi ya kupanda chakula na kukihifadhi kiwe cha manufaa hata kipindi cha kiangazi na njaa.

Wengi wa wakulima hao ni wale wanaohusika na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, kuku, viazi, ndizi, na mahindi.

Wakulima hao wanatoka maeneo ya Kikuyu, Limuru, Gatundu Kusini kaskazini, na Lari.

Dkt James Nyoro amesema maafisa wa kilimo kutoka Kaunti ya Kiambu watakuwa wakiwatembelea wakulima hao ili kuwapa motisha na matumizi ya teknolojia ya kisasa.

wakulima wamehimizwa kuzingatia kutumia mbolea ya kisasa ili kuongeza mapato zaidi kwenye kilimo chao.

Ili kufanikisha mpango huo wakulima hao walishauriwa kujiweka kwa makundi.