Tanzania kufanya kilimo cha ndizi kuwa cha kibiashara
2021-08-16 07:37:55| cri

Serikali ya Tanzania imeweka mikakati ya kukuza kilimo cha ndizi kuwa kilimo cha biashara ili kuongeza uzalishaji pamoja na kukuza soko la kimataifa ili kuongeza pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na waziri wa kilimo Tanzania, Profesa Adolf Mkenda wakati alipotembelea mashamba ya wawekezaji ya maua, ndizi na makademia ambapo aliambatana na kamati ya bunge ya kilimo ,mifugo na maji ya Tanzania.

Amesema zipo baadhi ya nchi zimenufaika na kilimo hicho hivyo kikiendelezwa hapa Tanzania wakulima watapa fursa ya kuuza zao hilo kwenye masoko ya kimataifa.

Mkenda amesema mwishoni mwa mwaka huu watafanya mkutano na wadau wa ndizi nchini humo ikiwa ni pamoja na wanasayansi ,watafiti ,wataalamu wa masoko pamoja na kampuni za kusafirisha na kununua ndizi hapa nchni humo.

Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuangalia namna ya kuendeleza kilimo cha ndizi nchini humo  ili waongeze uzalishaji kwa ajili ya chakula na kwa ajili ya kuuza kwenye masoko ya Kimataifa.