Baa la njaa lanukia katika Pembe ya Afrika wakati ukame ukiendelea
2021-09-22 09:17:41| cri

Shirika la maendeleo la kiserikali la nchi za Afrika mashariki (IGAD) limesema Pembe ya Afrika ina uwezekano wa kukabiliwa na njaa na utapiamlo wa kiwango kikubwa katika robo ya mwisho ya mwaka huu kutokana na ukame kuendelea kwa muda mrefu.

Uchambuzi wa hivi karibuni wa IGAD umeonesha kuwa watu milioni 36.7 hadi 37.2 wa kanda hiyo wataathiriwa na baa la njaa kutokana na vurugu, matukio ya hali mbaya ya hewa na janga la COVID-19, hali zinazohitaji kuchukuliwa hatua za dharura ili kuzuia kutokea kwa msukosuko mbaya wa kibinadamu.

Mratibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika eneo la Afrika Mashariki Bw. David Phiri, alisema kuwa serikali za nchi husika zinapaswa kuwekeza katika mifumo ya kilimo inayohimili hali ya hewa, huduma za ugani, na mifumo ya tahadhari za mapema ili kupunguza athari za ukame wa mara kwa mara kwa maisha ya watu.

Kutokana na uchambuzi wa IGAD, nchi tatu za Pembe ya Afrika Sudan, Ethiopia na Sudan Kusini ni miongoni mwa maeneo kumi yenye ukosefu mkubwa zaidi wa usalama wa chakula duniani.