Wiki ya Utamaduni ya China na Nigeria yafunguliwa Nigeria
2021-09-23 09:24:06| cri

Wiki ya Utamaduni ya China na Nigeria imefunguliwa huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria tarehe 21 mwezi huu kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Nigeria na kuhimiza urafiki na maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili.

Balozi wa China nchini Nigeria Cui Jianchun alihutubia kwenye ufunguzi wa shughuli hiyo akisema China na Nigeria zimeungana mkono katika kuhimiza ushirikiano na kuheshimu maslahi ya upande mwingine katika miaka 50 iliyopita, na zimepata mafanikio tele yanayonufaisha watu wa nchi hizo mbili. Wiki hiyo ya utamaduni itainua zaidi kiwango cha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Katibu wa kudumu katika Wizara ya Habari na Utamaduni Ifeoma Anyangwutaku amesema miaka 50 iliyopita imeshuhudia mawasiliano na ushirikiano wa kina kati ya Nigeria na China katika mambo ya sanaa, usimamizi wa utamaduni na mafunzo kwa raslimali watu, na wiki hiyo ni tunda lingine muhimu la ushirikiano wa kiutamaduni kati ya nchi hizo mbili.