Guterres ataka kuwepo kwa usawa katika usambazaji wa chanjo
2021-10-25 09:47:41| cri

Mkutano wa 13 wa kilele wa afya duniani umeanza mjini Berlin, Ujerumani, ukiwa na kauli mbiu ya “mafunzo kuhusu virusi vya Corona”.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alihutubia ufunguzi wa mkutano huo akilaani “utaifa wa chanjo” na kitendo cha kuhodhi chanjo, na kutaka kuwepo kwa usawa katika usambazaji wa chanjo. Ameonya kuwa ukosefu wa usawa katika usambazaji chanjo una maana ya kuwa na vifo vingi, uharibifu mkubwa wa utaratibu wa afya na tatizo kubwa zaidi la kiuchumi.

Naye mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Ghebreyesus amesema inatarajiwa kuwa kila nchi itaweza kutimiza lengo la kuchanja asilimia 40 ya wananchi wake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, huku akitoa wito kwa nchi za kundi 20 kutoa msaada wa chanjo ili kusaidia nchi nyingine dhaifu.

Mkutano huo wa afya unaofanyika kwa siku tatu umehudhuriwa na watu elfu sita, na maofisa na wataalam 300 kutoka mashirika ya kimataifa na nchi mbalimbali watatoa hotuba.