Rais wa China ahutubia ufunguzi wa mkutano FOCAC
2021-11-30 09:26:15| CRI

Rais wa China ahutubia ufunguzi wa mkutano FOCAC_fororder_1128113735_16382045757421n

Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umefanyika huko Dakar, mji mkuu wa Senegal. Rais Xi Jinping wa China amehudhuria ufunguzi wa mkutano huo kwa njia ya video, na kutoa hotuba muhimu.

Kwenye hotuba yake, Rais Xi amesema huu ni mwaka wa 65 tangu China na Afrika zianzishwe uhusiano wa kidiplomasia, na katika kipindi hicho, pande hizo zimejenga urafiki wa kindugu usiovunjika katika mapambano dhidi ya ubeberu na ukoloni, kuanzisha njia maalum ya ushirikiano katika kujipatia maendeleo, kusaidiana vizuri wakati mabadiliko makubwa yanatokea, na kuweka mfano mzuri kwa kujenga aina mpya ya uhusiano wa kimataifa.

Rais Xi ametoa mapendekezo manne kuhusu kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya China na Afrika katika zama mpya, ambayo ni kushikilia mshikamano katika kukabiliana na janga la COVID-19, kuzidisha ushirikiano halisi katika masuala ya biashara, uwekezaji, kuondokana na umaskini, uchumi wa kidijitali, ujasiriamali wa vijana wa Afrika na maendeleo ya kampuni ndogo na yenye ukubwa wa kati, kukuza maendeleo yasiyoleta uchafuzi wa mazingira, na kulinda usawa na haki.

Rais Xi amesema, kufuatia mpango wa kwanza wa miaka mitatu wa “Malengo ya mwaka 2035 ya Ushirikiano kati ya China na Afrika”, China itashirikiana kwa karibu na Afrika kutekeleza kwa pamoja “miradi tisa,” ambayo ni China kusaidia Afrika kukabiliana na janga la COVID-19, kuisaidia Afrika kupunguza umaskini na kuendeleza kilimo, kukuza biashara kati ya China na Afrika na kuongeza uagizaji wa bidhaa za Afrika hadi kufikia dola bilioni 300 za kimarekani katika miaka mitatu ijayo, kuongeza uwekezaji barani Afrika, kuhimiza uvumbuzi wa kidijitali barani Afrika, kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira, kuisaidia Afrika kujenga uwezo, kuhimiza mawasiliano ya ustaarabu na watu, na kuisaidia Afrika kuimarisha amani na usalama.