Hali ilivyo ya sasa ya maingiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande mbili

Radio China Kimataifa

Katika miaka 30 toka mwaka 1949 hadi 1978, kutokana na mapambano makali ya kijeshi na hali wasiwasi ya kukabiliana kijeshi kwenye sehemu ya Mlango wa bahari wa Taiwan, mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili yalikomeshwa kimsingi, ambapo aina chache tu za bidhaa za mahitaji ya lazima kama vile dawa za mitishamba za China bara na nyinginezo zilisafirishwa hadi Taiwan kwa kupitia Hongkong, tena kiasi cha bidhaa hizo zilizosafirishwa ni kidogo.

Baada ya mwaka 1979, serikali ya China ilichukua hatua kadha wa kadha za kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi kati ya China bara na Taiwan, ambapo utawala wa Taiwan pia ulikuwa hauna njia nyingine ila tu kurekebisha sera yake ya kiuchumi na kibiashara inayohusika na China bara, na ulilegeza vizuizi vya mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba, 2003, thamani ya jumla ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia dola za kimarekani bilioni 309.18, miongoni mwake, thamani ya bidhaa zilizouzwa na China bara kwenye soko la Taiwan ilifikia dola za kimarekani bilioni 48.89, na thamani ya bidhaa zilizoagizwa na China bara kutoka Taiwan ilifikia dola za kimarekani bilioni 260.29, ambapo pengo la biashara lilifikia dola za kimarekani bilioni 211.4. Kuanzia mwaka 1991, China bara imekuwa chanzo kikuu cha urari kwa Taiwan. Wakati huo huo Taiwan ikawa moja kati ya sehemu zilizowekeza vitega uchumi vingi China bara.

Hivi sasa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan umeendelea katika hali maalum kama zifuatazo: Kwanza, uhusiano wa kiuchumi wa pande hizo mbili, kimsingi ni biashara isiyo ya moja kwa moja na wafanyabiashara wa Taiwan wanawekeza vitega uchumi kwenye China bara, pamoja na kuanzisha viwanda au mashirika halisi, kufanya mangiliano ya kisayansi na kiteknolojia, maingiliano ya kifedha na kutoa mafunzo kwa watu. Pili, kutokana na vizuizi vya utawala wa Taiwan, wafanyabiashara wa Taiwan bado wanawekeza vitega uchumi kwenye China bara kwa njia isiyo moja kwa moja, yaani wakitaka kuwekeza kwenye China bara wanapaswa kupitia kampuni zilizosajiriwa kwenye sehemu ya tatu, na wakiwekeza vitega uchumi chini ya dola za milioni moja wanaweza kupitia kampuni za Taiwan moja kwa moja, lakini vitega uchumi hivyo vinapaswa kuingia China bara kupitia sehemu ya tatu. Kutokana na utawala wa Taiwan kukataa mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara na China bara, hivyo biashara ya pande hizo mbili pia inaweza kufanyika kwa kupitia sehemu ya tatu. Na kutokana na utawala wa Taiwan kupiga marufuku uwekezaji wa China bara Kisiwani Taiwan, kumekuwepo kwa hali isiyo ya kawaida na biashara isiyo ya uwiano kati ya pande hizo mbili. Tatu, katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa kiuchumi wa kutegemeana wa pande hizo mbili unaimarishwa siku hadi siku, na hali ya kusaidiana na kunufaishana inaonekana dhahiri siku hadi siku.