Ziwa la Kanasi

中国国际广播电台

      Ziwa la Kanasi liko katika wilaya ya Buerjin iliyoko katika sehemu ya kaskazini yenye umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu wa wilaya. Ziwa hilo liko ndani ya msitu mnene kwenye sehemu ya juu ya mlima likiwa na urefu wa mita 1374 juu ya usawa wa bahari, eneo la ziwa hilo ni kilomita za mraba 45.73 na sehemu yenye maji mengi zaidi ina kina cha mita 188.5.
Pembezoni mwa ziwa la Kanasi ni milima mirefu yenye barafu na theluji, mandhari yake ya asili inapendeza sana. Sehemu hiyo ni ya pekee nchini China yenye wanyama na mimea ya sehemu ya Siberia ya Kusini vikiwa na miti aina karibu 800 ikiwemo miti adimu ya spruce, fir na Korean pine, aina 39 za wanyama, aina 117 za ndege, wanyama wanaotambaa na kuweza kuishi ndani ya maji aina 4, aina 7 za samaki na wadudu aina zaidi ya 300, ambazo aina nyingi zake ziko katika sehemu hiyo tu. Sehemu hiyo ina mandhari nzuri ya mbuga yenye misitu kati yake, maziwa mengi na yenye thamani kubwa ya utalii, hifadhi ya mazingira ya asili, utafiti wa sayansi, historia na utamaduni.