Wanawake hodari kwenye jukwaa la kisiasa
Radio China Kimataifa
 

       Song Qingling:

 Song Qingling (1893- 1981) mwanasiasa, mwanaharakati wa mambo ya kijamii, kiongozi mmoja muhimu wa Jamhuri ya watu wa China. Alihitimu mwaka 1913 katika Chuo Kikuu cha wanawake cha Wesleyan cha Macon cha Jimbo la Georgia la Marekani. Mwaka 1915 aliolewa na Bwana Sun Yat-sen. Baada ya Bw Sun Yat sen kufariki dunia mwaka 1925, alishikilia sera tatu za kisiasa zilizotolewa na mume wake za kujiunga na nguvu ya mapindizi ya Urusi, Chama cha Kikomunisti cha China na kuwasaidia wakulima na wafanyakazi. Mwaka 1927 na 1929 aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa heshima wa Chama cha Muungano cha Kimataifa cha Kupinga Ubeberu, na kuwa mmoja wa viongozi muhimu wa kamati ya kupinga ufashisti duniani. Mwaka 1931 alirudi China, na kushughulikia kwenye kazi ya utoaji wa huduma za jamii, kushiriki kwenye shughuli za kupambana na wavamizi wa Japan na kuokoa taifa la China, kukosoa sera za serikali ya Chama cha Guomintang za kusalimu amri kwa Japan, na kuwakandamiza wananchi. Mwishoni mwa mwaka 1932, alianzisha Shirikisho la kulinda haki za wananchi wa China, na kujaribu kuwaokoa wanamapinduzi waliopigania haki za kidemokrasia. Mwaka 1933 Bi. Song Qingling aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la China la Shirikisho la Kupinga Ubeberu na Vita la Mashariki ya Mbali. Baada ya kutokea vita dhidi ya wavamizi wa Japan, Bi. Song Qingling alianzisha Shirikisho la Kuilinda China huko Hongkong, na kuchangisha zana za matibabu kuwaunga mkono wananchi wa China katika mapambano dhidi ya wavamizi wa Japan.

Mwezi Septemba mwaka 1945, baada ya China kupata ushindi katika vita dhidi ya wavamizi wa Japan, Bi. Song Qingling alitoa mwito na kuwataka wananchi wa Marekani kuipinga serikali ya Marekani isimuunge mkono Chiang Kai-shek kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Alianzisha Mfuko wa Utoaji Huduma wa China, kushughulikia mambo ya wanawake na watoto. Bi. Song Qingling aliteuliwa kuwa naibu mwenyekiti wa serikali kuu baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, baadaye alichaguliwa kwa nyakati tofauti kuwa naibu mwenyekiti wa taifa, naibu spika wa Bunge la Umma la China, mwenyekiti wa heshima wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China na mwenyekiti wa Kamati ya Kuwalinda Watoto ya China. Mwaka 1950 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Amani Duniani, na kupata tuzo ya Stalin kutokana na mchango wake katika kuimarisha amani ya kimataifa mwaka 1951. Mwaka 1952, Bi. Song Qingling aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ya Amani ya Asia na Pasifiki.

  Cai Chang  

 Bibi Cai Chang (1900-1990), Mzaliwa wa mkoa wa Hunan, alikuwa naibu spika wa Bunge la awamu ya 4 na 5 la umma la China. Alikuwa mwanamapinduzi maarufu wa tabaka la wafanyakazi, mwanzilishi na kiongozi hodari wa harakati za wanawake wa China, pia alikuwa mwanaharakati maarufu wa harakati za wanawake wapendao maendeleo ya kimataifa.

Bi. Cai Chang aliwahi kusoma nchini Ufaransa. Mwaka 1923 alijiunga na Chama cha Kikomunisti cha China. Mwezi Octoba mwaka 1934 alishiriki katika safari ndefu za kilomita elfu 25. Baada ya kuasisiwa kwa China mpya mwaka 1949, Bi. Cai Chang aliteuliwa kwa nyakati tofauti kuwa mwenyekiti wa awamu ya kwanza, pili na tatu wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China, mwenyekiti wa heshima wa awamu ya nne wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China. Alikuwa mjumbe wa vikao vinne vya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, mjumbe wa kudumu wa Bunge la Umma la China la awamu tatu mfululizo, na naibu spika wa Bunge la Umma la China la awamu ya nne na tano.

  Deng Yingchao

 Deng Yingchao (1904-1992) alikuwa mwanamapinduzi wa tabaka la wafanyakazi, mwanasiasa, mwanaharakati maarufu wa mambo ya kijamii na mwanzilishi wa harakati za wanawake nchini China. Maskani yake ya kiasili ni mkoa wa Henan, alizaliwa huko Nanning, mkoani Guangxi. Mwaka 1919 alishiriki harakati ya "Tano Nne" ya kupambana na ubeberu na ukabaila, kuandaa na kuongoza harakati za uzalendo za wanafunzi wa Tianjin pamoja na Zhou Enlai na viongozi wengine. Mwaka 1925 aliolewa na Zhou Enlai, na kujiunga na safari ndefu za kilomita elfu 25. Bi. Deng aliwahi kuteuliwa kuwa mkuu wa tawi la China la harakati za Kimataifa za kupambana na uvamizi. Baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, aliteuliwa kwa nyakati tofauti kuwa naibu mwenyekiti, naibu katibu mkuu, na mwenyekiti wa heshima wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China, naibu mwenyekiti wa Kamati ya Kulinda Watoto ya China, na mkuu wa heshima wa Shirikisho la Urafiki na nchi za Nchi za Nje. Bi. Deng aliwahi kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China kwa awamu tano mfululizo, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Kamati Kuu kwa awamu mbili, katibu mkuu wa pili wa Kamati ya Ukaguzi wa Nidhamu ya Kamati Kuu. Bi. Deng pia aliwahi kuteuliwa kuwa mjumbe na naibu spika wa Bunge la Umma la China, mjumbe na mwenyekiti wa Halmashauri ya Mashauriano ya Kisiasa ya China.

   Shi Liang 

Bi. Shi Liang (1900-1985), mzaliwa wa mji wa Changzhou, mkoani Jiangsu. Aliteuliwa kuwa naibu spika wa awamu ya 5 na 6 wa Bunge la Umma la China, naibu mwenyekiti wa awamu ya 5 cha baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, waziri wa kwanza wa sheria wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Bi. Shi Liang alikuwa mwanzilishi na kiongozi mmojawapo wa harakati za wanawake nchini China, mwanasiasa na mwanasheria. Mwaka 1931, Bi. Shi Liang alianza kufanya kazi ya uwakili. Mwaka 1936 alikamatwa na serikali ya Chama cha Guomintang cha China kutokana na kuongoza harakati za kupambana na wavamizi wa Japan na kuliokoa taifa la China. Baada ya kuzaliwa kwa China mpya, aliteuliwa kuwa waziri wa kwanza wa sheria wa China na mjumbe wa Kamati ya Kisiasa na Kisheria ya Baraza la Mawaziri la China. Kwa nyakati tofauti aliteuliwa kuwa mwakilishi, mjumbe wa kudumu na naibu spika wa Bunge la Umma la China, mjumbe wa kudumu, na naibu mwenyekiti wa baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, na naibu mkurugenzi wa Kamati ya Utungaji Sheria. Pia aliteuliwa kwa nyakati tofauti kuwa mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, naibu mwenyekiti na mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Chama cha Muungano wa Kidemokrasia, na naibu mwenyekiti wa Shirikisho Kuu la Wanawake la China.


  Wu Yi 

 Wu Yi (1938-), naibu waziri mkuu wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Mzaliwa wa Wuhan, mkoani Hubei. Bi. Wu Yi ni mhitimu wa shahada ya usafishaji wa mafuta ya Chuo Kikuu cha Mafuta cha Beijing, ni mhandisi mkuu. Alijiunga na Chama cha Kikomunisti cha China mwezi Aprili mwaka 1962. Aliwahi kuwa fundi wa karakana, na naibu mkuu wa kiwanda. Kuanzia mwaka 1983 hadi 1988 alikuwa naibu meneja na katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti katika Kampuni ya Kemikali ya Mafuta ya Yanshan, Beijing. Mwaka 1988-1991, aliteuliwa kuwa naibu meya wa Beijing. Kuanzia mwaka 1991 hadi 1993, alikuwa naibu waziri na naibu katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China kwenye Wizara ya Uchumi na Biashara kwa Nchi za Nje. Mwaka 1993 aliteuliwa kuwa waziri na katibu mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Uchumi na Biashara kwa Nchi za Nje. Mwaka 1998-2003, aliteuliwa kuwa mjumbe wa taifa. Mwezi Machi mwaka 2003, aliteuliwa kuwa naibu waziri mkuu. Mwezi Aprili mwaka 2003 alishika cheo kingine cha waziri wa afya. Bi. Wu Yi kwa nyakati tofauti aliteuliwa kuwa mjumbe mbadala na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, mjumbe mbadala na mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomusniti cha China.