Hakikisho la afya kwa wanawake wa China
Radio China Kimataifa
 

Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya afya ya wanawake wa China imeboreshwa kidhahiri. Ilipofika mwaka 2002, asilimia 86 ya wajawazito wa China walipewa huduma za afya, na asilimia 78.8 ya wajawazito walijifungua hospitalini, na kiasi cha wajawazito waliokufa wakati wa kujifungua kilipungua sana. Wastani wa maisha ya wanawake ni miaka 73.6, ukiwazidi wanaume kwa miaka 3.8.

China imeanzisha mtandao wa huduma za afya vijijini. Kuanzia mwaka 2000 hadi 2001, serikali kuu na serikali za mikoa zilianzisha harakati ya kupunguza vifo vya wajawazito na kutokomeza hali ya watoto wachanga kupata ugonjwa wa pepo punda katika mikoa, miji na mikoa inayojiendesha ya magharibi mwa China, kuimarisha ujenzi wa hospitali za uzazi katika vitongoji vilivyoko katika sehemu maskini, na kuwaandaa wafanyakazi wa sekta ya afya.

Mwezi Aprili mwaka 2001, baraza la serikali lilitoa "utaratibu wa kutekeleza sheria ya afya ya mama na watoto wachanga ya Jamhuri ya Watu wa China", ikidhihirisha zaidi huduma zinazopaswa kutolewa kwa wanawake na watoto, kuimarisha kazi ya kupima na kutibu maradhi ya wanawake nchini. Ilipofika mwaka 2002, vituo 3067 vya afya vya wanawake na watoto vilianzishwa nchini kote.

Serikali ya China inatilia maanani sana kazi ya kinga na tiba ya ugonjwa wa ukimwi, ikiwa imetunga "mpango wa kipindi kirefu na cha wastani wa kinga na tiba ya ukimwi"(1998-2010) na "mpango wa kuzuia na kutibu ukimwi wa China" (2001-2005). Serikali katika ngazi tofauti zinafuatilia sana kueneza ujuzi kuhusu jinsi ya kukinga ukimwi na magonjwa ya zinaa, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama wazazi hadi kwa watoto.