Miradi ya Wanawake ya Ushirikiano wa Kimataifa
Radio China Kimataifa
 

Kutokana na kuimarishwa kwa maingiliano kati ya wanawake wa China na wa nchi za nje, mashirika mengi zaidi na zaidi ya wanawake wa China yameanza kutumia miradi ya ushirikiano ya kimataifa na nadharia ya kimaendeleo ya kimataifa kutatua masuala halisi ya wanawake wa China. Katika miaka 5 iliyopita, Shirikisho Kuu la Wanawake la China limefanya miradi ya ushirikiano na mashirika mengi ya kimataifa, kutoa mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kuishi na kujiendeleza kwa wanawake na watoto wa China kwa kuboresha afya ya wanawake, kutokomeza hali ya kutojua kusoma wala kuandika na kutoa mikopo mdogo. Shirikisho Kuu la Wanawake la China limesifiwa sana na mashirika ya kimataifa kwa ufanisi mkubwa na uaminifu.

Katika miaka ya hivi karibuni, mashirika ya wanawake ya China yameanzisha miradi mingi ya ushirikiano na jumuiya husika za wanawake za kimataifa, mashirikisho hayo ni pamoja na: "Mradi wa sheria ya wanawake kati ya China na Canada" (mwaka 1998). Huu ni mradi wa ushirikiano unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa ya Canada na kutekelezwa kwa pamoja na Shirikisho Kuu la Wanawake la China na Chuo Kikuu cha Mitaa cha Canada. Mradi huo unalenga kutekeleza vizuri zaidi sheria na taratibu husika kuhusu haki na maslahi ya wanawake, na kulinda haki za wanawake kwa kuinua mwamko na uwezo wao wa kutumia sheria, kuinua mwamko wa kijinsia wa wanasheria na uwezo wa mashirika ya wanawake wa kueneza sheria na kuwaelimisha wanawake. Wanawake wengi wa sehemu inayotekeleza mradi huo wameanza kujua jinsi ya kulinda haki na maslahi yao kwa kutumia sheria.

Miradi mingine ya ushirikiano kati ya jumuiya za wanawake wa China na ya kimataifa ni kama vile "mradi wa kupinga na kuzuia uuzaji wa wanawake na watoto wa sehemu ya delta ya mto Mekong" na "mradi wa kuwasaidia wanawake waliopunguzwa kazini kupata ajira mpya".

Shirikisho Kuu la Wanawake la China pia limefanya ushirikiano na Shirika linaloshughulikia Mambo ya Watoto la Umoja wa mataifa UNICEF, idara ya maendeleo ya kimataifa ya Uingereza na mashirika mengine kuhusu watoto wa kike. Miradi hiyo inalenga kubadili mitizamo na mienendo mibaya ya watu ya kuwabagua watoto wa kike, kuwasaidia watoto wa kike wawe na uwezo wa kujishirikisha katika maendeleo ya uchumi na jamii na kujua jinsi ya kulinda haki na maslahi yao.

Tokea mwaka 1999, miradi ya ushirikiano wa kimataifa imesaidia kujenga shule nyingi za msingi au madarasa kwa ajili watoto wa kike ili kuwawezesha watoto wa kike wa China waliolazimika kuacha shule kutokana na matatizo ya kiuchumi warudi shuleni.