Enzi ya Ming
中国国际广播电台
Mwaka 1368 Zhu Yuanzhang alikuwa mfalme katika mji wa Nanjing na kuanzisha enzi ya Ming. Kwa muda wa miaka 31 tangu awe mfalme, mfalme Ming Taizu aliimarisha madaraka ya udikteta wa kimwinyi, kuua mawaziri wenye mafanikio na wapinzani ili kuimarisha utawala wake. Baada ya mfalme Ming Taizu kufariki, mjukuu wake Jianwen alirithi ufalme, lakini alishindwa kwa jeshi la baba yake mdogo. Tokea hapo Zhuli akawa mfalme na kujiita kuwa Ming Chengzu. Mwaka 1421 alihamishia mji mkuu mjini Beijing.

Ingawa enzi ya Ming iliimarisha madaraka ya kifalme, lakini wafalme wengi ama walikuwa mbumbumbu au walikuwa bado watoto na kutoshughulikia mambo ya nchi, hivyo madaraka yalitwaliwa na watumishi wa jumba la mfalme, ambao walitamani mali, kuwaua mawaziri adilifu na kusababisha mgongano wa kijamii. Ingawa wakulima walifanya uasi mara kadhaa katikati ya kipindi cha enzi ya Ming, lakini wote walikandamizwa.

Katika enzi ya Ming alikuwepo mwanasiasa mashuhuri Zhang Juzheng, aliyefanya mageuzi ili kupunguza mgongano wa kijamii na kuimarisha nguvu ya utawala wa enzi ya Ming.

Kilimo kilikuwa na maendeleo makubwa zaidi katika enzi ya Ming kuliko enzi za zamani, ambapo sekta nyingine za nguo, vyombo vya kauri, uchimbaji wa madini ya chuma, utengenezaji wa vyombo vya shaba, karatasi na uundaji wa marikebu pia vilipata maendeleo. Katika enzi ya Ming uhusiano wa kiuchumi na kiutamaduni ulikuzwa. Msafiri mkubwa Zheng He alisafiri mara 7 baharini hadi nchi na sehemu zaidi ya 30 za Asia na Afrika. Lakini baada ya hapo, Enzi ya Ming ilivamiwa na Japan, Hispania, Ureno na Uholanzi.

Katika kipindi cha mwisho cha enzi ya Ming, jamaa za wafalme na majemedari walikuwa na mashamba mengi, kodi za serikali pia zilikuwa nyingi, hali hiyo ilisababisha mgongano mkubwa wa kijamii. Baadhi ya maofisa walitarajia kupunguza mgongano wa kijamii, wakidai kudhibiti haki maalumu za watumishi wa jumba la mfalme na mabwenyenye, lakini walikandamizwa na wenye madaraka, hali ambayo ilizidisha hali ya wasiwasi.

Mwaka 1627 yalitokea maafa ya makubwa ya kimaumbile, lakini maofisa waliwalazimisha wakulima kulipa kodi, jambo ambalo lilisababisha wakulima kufanya uasi. Mwaka 1644 jeshi la wakulima liliuteka mji wa Beijing, na mfalme Chongzhen alijiua.