Enzi ya Qing
中国国际广播电台
Enzi ya Qing ilikuwepo kuanzia mwaka 1644 hadi mwaka 1911, muda ambao kulikuwa na wafalme 12 na kutawala China kwa miaka 268.

Enzi ya Qing ilipokuwa na nguvu kubwa kabisa ilikuwa na ardhi yenye eneo la kilomita za mraba milioni zaidi ya 12. Mwaka 1616 Nuerhachi alianzisha enzi ya Jin ya pili, mwaka 1636 mfalme Huangtaiji alibadilisha jina la nchi kuwa Qing. Mwaka 1644 jeshi la wakulima lililoongozwa na Li Zicheng liliangusha enzi ya Ming, mfalme Chongzhen wa enzi ya Ming alijiua. Jeshi la Qing liliingia sehemu ya kati ya China na kutumia nafasi hiyo kulishinda jeshi la wakulima na kuuchukua Beijing kuwa mji mkuu wa Qing. Enzi ya Qing ilivunjilia mbali majeshi ya wakulima yaliyokuwa kwenye sehemu mbalimbali za China na kuunganisha sehemu zote za China hatua kwa hatua.

Ili kupunguza mgongano wa kijamii, mwanzoni enzi ya Qing ilihamasisha wakulima kufyeka mashamba na kutekeleza sera za kupunguza kodi, hatua hiyo iliyochukuliwa ilileta maendeleo ya jamii na uchumi kwenye sehemu za ndani na mipakani. Ilipofika katikati ya karne ya 18, uchumi wa enzi ya Qing ulikuzwa zaidi na kufika kileleni, nguvu ya nchi ilikuwa kubwa, utaratibu wa jamii ulikuwa shwari, na idadi ya watu ilifikia kiasi cha milioni 300.

Mwaka 1661 Zheng Chenggong aliongoza kundi la manowari kuvuka mlango bahari wa Taiwan na kuwashambulia wakoloni wa uholanzi waliokalia Taiwan kwa miaka 38. Mwanzoni mwa mwaka uliofuata, wakoloni wa Uholanzi walisalimu amri, na Taiwan ilirejea China.

Katika miaka ya mwisho ya karne ya 16 Urusi ya Tsar ilijipanua kwa sehemu ya mashariki. Wakati jeshi la Qing lilipoingia sehemu ya kati ya China, mfalme Tsar wa Urusi alitumia nafasi hiyo kukalia sehemu kadhaa zikiwemo Yaksa na Nibuchu. Serikali ya Qing ilitaka wavamizi wa Urusi waondoke kutoka ardhi ya China. Mwaka 1685 na mwaka 1686 mfalme Kangxi aliamuru jeshi la Qing kushambulia jeshi la mfalme Tsar wa Urusi lililoko Yaksa, ambapo lililazimika kukubali kutatua suala la mpaka wa sehemu ya mashariki kati ya China na Urusi kwa njia ya mazungumzo. Mwaka 1689, wawakilishi wa China na Urusi walikuwa na mazungumzo huko Nibuchu na kusaini rasmi “mkataba wa mpaka wa Nibuchu”.

Katika kipindi cha kati cha enzi ya mfalme Qianlong, serikali ilituliza kundi la wafarakanishaji la Geerdan wa sehemu ya Zhungeer na uasi uliofanywa na kabila la wahui, kuunganisha sehemu zote za Xinjiang na kutekeleza sera kadhaa za kuhimiza uchumi, utamaduni na mawasiliano ya sehemu ya mpakani.

Kabla ya kipindi cha mfalme Daoguang, enzi ya Qing ilipata maendeleo makubwa katika mambo ya utamaduni, ambapo walijitokeza waandishi wakubwa wa vitabu na vitabu vikubwa mashuhuri. Vilevile maendeleo mengi katika eneo la sayansi na teknolojia hususan katika sekta ya ujenzi wa majengo.

Mwaka 1840 vilizuka vita vya kasumba, baada ya hapo nchi za kibeberu ziliishambulia China, ambapo utawala wa enzi ya Qing ulisaini mikataba mingi isiyo ya haki, kuzipa ardhi, kutoa fidia na kufungua milango ya miji ya pwani kwa shughuli za biashara, Jamii ya China ilibadilika hatua kwa hatua kuwa nchi ya nusu kimwinyi na nusu ya kikoloni. Katika kipindi cha miaka ya mwisho siasa ya enzi ya Qing ilijaa ufisadi, kushikilia wazo lile la kizamani, kuwa waoga na unyonge na kuzorota mwaka hadi mwaka. Watu wa China waliishi kwa taabu kubwa walianzisha harakati za kupinga ubeberu na umwinyi. Ili kujiokoa watawala walifanya baadhi ya mageuzi wakijaribu kufanya China kushika njia ya ustawi, lakini hatimaye walishindwa kabisa. Mashujaa wengi walipigana vita kufa na kupona wakijitahidi kuiokoa China. Mwaka 1911 yalitokea mapinduzi ya Xinhai ambayo yaliuangusha utawala wa enzi ya Qing na kumaliza utaratibu wa kimwinyi uliodumu kwa miaka zaidi ya 2,000, tokea hapo China iliingia katika kipindi kipya.