Kaburi la mfalme Qinshihuang
中国国际广播电台
Kaburi la mfalme Qinshihuang liko kwenye tarafa ya Yanzhai, umbali wa kilomita 5 upande wa mashariki wa mji mkuu wa wilaya ya Lintong mkoani Shanxi. Ukiangalia kutoka angani, kaburi hilo linaonekana kama piramidi kubwa. Eneo la kaburi hilo lina kilomita za mraba 66.25, ambalo ni kubwa kwa zaidi ya mara 2 kuliko eneo la mji wa Xian wa hivi sasa.

 Tangu aliporithi ufalme alipokuwa na umri wa miaka 13, mfalme Qinshihuang alianza kujijengea kaburi kwenye mlima wa Li, baada ya kuunganisha nchi nyingine 6, alikusanya watu zaidi ya laki moja kutoka sehemu mbalimbali kuendelea kumjengea kaburi, ujenzi uliendelea kwa miaka 37 hadi alipokufa akiwa na umri wa miaka 50.
Kitabu cha historia kinasema kuwa jumba la kuwekea maiti ya mfalme Qinshihuang lilichimbwa chini ya chemchemi na kuimarishwa kwa maji ya madini ya shaba, ndani yake viliwekwa vito na vitu vingine vyenye thamani. Ili kuzuia wezi kuingia ndani ndani ya jumba la kaburi iliwekwa upinde na mishale mingi, ambayo inajirusha yenyewe wakati inapoguswa. Pembeni mwa kaburi ziliwekwa sanamu nyingi za askari na farasi. Usanifu wa kaburi ulizingatia kuonesha madaraka na heshima ya mfalme huyo.

Kutokana na “Kitabu cha Han” na kitabu cha “Maelezo ya Shuijing”, kaburi la mfalme Qinshihuang lilitobolewa na Xiang Yu mwaka 206 kabla ya Kristu. Xiang Yu alipeleka askari laki 3 na kusafirisha vitu vilivyokuwemo ndani ya kaburi kwa siku 30.
Lakini wako baadhi ya watu wanaosema kuwa mwandishi maarufu wa “Kitabu cha Historia” aliandika makala maalumu kuhusu mfalme Qinshihuang, lakini hakueleza hata neno moja kuhusu kuharibiwa kwa kaburi la mfale Qinshihuang, lakini mwandishi wa kitabu cha “Maelezo ya Shuijing” aliandika maelezo kamili katika miaka 600 hapo baadaye kuhusu matukio hayo, ambayo yanatia watu mashaka.
Baada ya mwaka 1949, watafiti wa mabaki ya kale wa China walifanya uchunguzi juu ya kaburi la mfalme Qinshihuang, hususan baada ya kugunduliwa kwa sanamu ya askari na farasi. Watafiti hao walitoboa matundu zaidi ya 200, waligundua matundu mawili yaliyochimbwa na wezi, ambayo yalikuwa na kipenyo cha sentimita 90 na urefu wa kwenda chini kwa mita 9, lakini matundu hayo mawili yako kwenye umbali wa mita 250 kutoka sehemu ya katikati ya kaburi, na wote hawakuingia katika jumba lililoko chini ya ardhi. Hivyo, maelezo yaliyoandikwa na Li Daoyuan kuhusu Xiang Yu kuchimba kaburi si ya kweli. Inakisiwa kuwa vitu walivyochukua akina Xiang Yu vilikuwa vitu vilivyoko katika majengo mengine ya kaburi la mfalme Qinshihuang. Kama hali halisi ni kama ilivyokisiwa, basi kaburi la mfalme Qinshihuang litakuwa jumba la kwanza kwa ukubwa duniani lililoko chini ya ardhi.