Mshairi Du Fu
中国国际广播电台


     Katika historia ya fasihi ya China watu hutaja washairi wawili wakubwa Li Bai na Du Fu kuwa ni wawakilishi wa mafanikio makubwa ya uashairi katika Enzi ya Tang (618-907).

Du Fu alizaliwa mwaka 712, alikuwa ni mjukuu wa mshairi mashuhuri Du Shenyan. Du Fu alikuwa mtoto mwenye kipaji kisicho cha kawaida. Toka utotoni mwake alikuwa na hamu ya kujifunza na alipokuwa na umri wa miaka 7 alianza kutunga mashairi. Baada ya kuwa mtu mzima alikuwa hodari wa kuchora picha, kupanda farasi na kucheza kitara. Tokea alipokuwa na umri wa miaka 19 alianza kutembelea huku na huko kwenye mandhari nzuri ya mito na milima na alipata kuona mengi, wakati huo kilikuwa ni kipindi cha ustawi kabisa cha Enzi ya Tang.

Kama walivyokuwa wasomi wengi wengine wa China, Du Fu pia alitamani kuwa na wadhifa fulani katika utawala wa kifalme, mara nyingi alikuwa anawasifu watu wenye madaraka na matajiri lakini hakupata chochote. Alipokuwa mtu wa makamo aliishi maisha ya kimaskini katika mji mkuu wa Enzi ya Tang, Chang An, na alishuhudia hali ya kusikitisha ya watu maskini kufa kwa njaa na baridi huku matajiri wakiishi maisha ya anasa, aliandika kifungu kinachojulikana kwa wote hadi leo, “Nyama na pombe zaoza nyumbani kwa matajiri, watu maskini wanakufa mitaani”. Maisha yake magumu yalimfanya aelewe kwa kina ufisadi wa watawala na janga la watu maskini, na kumfanya awe mshairi anayehangaikia sana hali ya taifa na wananchi.

Mwaka 755 Du Fu alipokuwa na umri wa miaka 43 alipata wadhifa, lakini baada ya mwezi mmoja vita vilizuka na kuendelea kwa muda mrefu. Katika kipindi hiki Du Fu alizurura zurura akiwa na maisha magumu na alikuwa ametambua vema jamii aliyoishi na aliandika mashairi mengi maarufu.

Mwaka 759 alikuwa amekata tamaa kabisa kuhusu siasa, aliacha wadhifa wake. Wakati huo kulitokea ukame na maisha yake yalikuwa ya kimaskini kabisa na hata alishindwa kuendelea na maisha yake, aliwaongoza jamaa yake kwenda kwenye mji uliopo katika sehemu ya kusini magharibi ya China. Kutokana na msaawa wa marafiki zake aliishi kwa miaka minne bila kuwasiliana na wengine, wakati huo aliandika shairi maarufu la kuelezea maisha yake magumu la “Nyumba Iliyoezeuliwa paa na Upepo”, akionesha matumaini yake ya kukubali kulala mitaani kama angeweza kuwapatia watu wote nyumba ili wajihifadhi kwenye ya kuhifadhi kwenye joto.

Du Fu alifariki mwaka 770 alipokuwa na umri wa miaka 59 kutokana na umaskini na ugonjwa akiwa katika safari ya kuzurura. Mashairi ya Du Fu yaliyobaki sasa yako 1400, kwa kina yameonesha miaka 20 hali ya jamii yenye vurugu ya vita, kutoka ustawi hadi kuporomoka kwa uchumi katika Enzi ya Tang.