Mshairi Li Bai
中国国际广播电台


    Li Bai alizaliwa mwaka 701 na kufariki dunia mwaka 762, alikuwa mwenyeji wa mkoa wa Gansu wa leo. Hadi sasa haijafahamika kama alizaliwa katika ukoo gani, lakini kutokana na mashairi yake tunaweza kufahamu kuwa yeye alizaliwa katika ukoo wenye hali nzuri kiuchumi na kiutamaduni. Tokea alipokuwa mtoto alipenda kusoma na alisoma vitabu vingi. Tangu alipokuwa na miaka 20 alianza kutembelea kila mahali ili kuona mengi. Kutokana na elimu yake kubwa na akili yake timamu, alifanikiwa sana katika uandishi wa mashairi. Ingawa wakati huo hali ya uchapaji na mawasiliano ilikuwa duni, lakini kupitia maingiliano ya wasomi jina lake lilijulikana sana.

Kusoma ili kujipatia nyadhifa ni tumaini la wasomi wote katika enzi za kale za China. Li Bai alipokuwa kijana alikuwa na tumaini kubwa la kupata wadhifa, kutokana na lengo hilo alikwenda mji mkuu wa Enzi ya Tang, Changan. Kutokana umaarufu wake na kupendekezwa na wasomi, mwaka 742 alichaguliwa kuwa afisa katika kasri la mfalme. Huu ulikuwa ni wakati mzuri kabisa maishani mwake.

Li Bai alikuwa ni mtu mwenye kiburi, alikuwa na malalamiko mengi kuhusu ufisadi na alitamani kuthaminiwa zaidi na mfalme, ili aoneshe uhodari wake katika mambo ya siasa, lakini mfalme alimchukulia kama ni mshairi aliyetumiwa tu wakati mfalme anapokuwa na haja naye. Li Bai alikata tamaa, na aliondoka mji mkuu Changan na kuanza tena maisha ya kutembea tembea kila mahali akiwa anajifariji kwa kunywa pombe na kuandika mashairi.

Mashairi ya Li Bai yaliyobaki hadi sasa ni zaidi ya 900.