中国国际广播电台
Enzi ya Tang ni kipindi muhimu
katika historia ya China. Katika
kipindi hicho uchumi ulistawi,
jamii ilikuwa tulivu, utamaduni
na sanaa viliendelea kwa haraka
na hasa mashairi yalikuwa yamepamba
moto. Kutunga mashairi kulikuwa
ni maisha muhimu ya wasomi katika
Enzi ya Tang. Kitabu kiitwacho
“Mkusanyiko wa Mashairi ya Enzi
ya Tang” kimekusanya mashairi
karibu elfu 50 yaliyoandikwa
na washairi zaidi ya elfu mbili
na mia tatu.
Maendeleo ya mashairi ya
Enzi ya Tang yanaweza kugawanyika
katika vipindi vinne vya enzi
hiyo, navyo ni kipindi cha
mwanzo, kipindi cha ustawi,
kipindi cha katikati na kipindi
cha mwisho.
Kipindi cha mwanzo (618—712).
Katika kipindi hiki waliibuka
“washairi hodari wanne”, nao
ni Wang Bo, Yang Jong, Lu
Jielin na Luo Binwang ambao
waliweka kanuni za mashairi
ya kale yenye mistari maalumu
na kila mstari uwe na maneno
maalumu yaani maneno matano
au maneno saba. Kutokana na
juhudi zao mashairi hayakuwa
ya burudani tena ndani ya
kasri la kifalme, bali yamekuwa
yakieleza maisha halisi ya
wananchi.
Kati ya mwaka 712 hadi mwaka
762 kilikuwa ni kipindi cha
ustawi cha Enzi ya Tang. Katika
kipindi hiki uandishi wa mashairi
ulipamba moto. Kulikuwa na
mada nyingi za mashairi zikielezea
uzuri wa maumbile, kusifu
mashujaa na kueleza hisia
za masikitiko. Washairi walikuwa
wakiandika mashairi katika
mazingira ya uhuru na kukifanya
kipindi hiki kifikie kilele
cha mashairi katika historia
ya China.
Katika kipindi hiki cha
ustawi cha Enzi ya Tang, washairi
wakubwa walikuwa ni Li Bai,
Du Fu, Wang Wei, Meng Haoran,
Gao Shi na Cen Can. Kati ya
hao Li Bai na Du Fu ndio wawakilishi
wa washairi wa kipindi hiki,
mashairi yao yameathiri sana
mashairi ya hapo baadaye.
Katika kipindi cha Katikati
cha Enzi ya Tang (762—872)
washairi walio maarufu zaidi
ni Bai Juyi, Yuan Zhen na
Li He. Bai Juyi alikuwa hodari
wa kuandika mashairi ya kudhihaki
utawala wa kutoza kodi kubwa,
kupinga vita na kuwaponda
matajiri wenye madaraka, na
alijitahidi kutumia lugha
rahisi. Mashairi yaliwapendeza
sana wasomaji.
Li He alikuwa na maisha
mafupi, aliishi zaidi ya miaka
20 tu. kutokana na kuwa maisha
yake yalikuwa magumu na tumaini
lake liligongwa mwamba, mashairi
yake yalijaa huzuni.
Kipindi cha mwisho cha Enzi
ya Tang (827—859) ni kipindi
ambapo cha washairi Li Shangyin
na Du Mu walikuwa katika kilele
cha kuandika mashairi. Mashairi
ya Du Mu, mengi yalikuwa yakionesha
nia yake ya kisiasa, na mashairi
ya Li Shangyin mengi yalikuwa
yakionesha masikitiko na simanzi
kutokana na usumbufu wake
alipokuwa na wadhifa.
|