Qu Yuan na Mashairi Yake
中国国际广播电台

Qu Yuan ni mshairi anayependwa na kuheshimiwa sana na Wachina. Mshairi huyo aliishi katika Kipindi cha Madola Yaliyopigana Vita (475 K.K.—221 K.K.). Katika kipindi hicho madola madogo madogo yalikuwa mengi, na yalipigana vita miaka hadi miaka. Kati ya madola hayo, Dola la Qin na Chu yalikuwa na nguvu zaidi, madola mengine yalikuwa yakifuata madola hayo mawili.

Qu Yuan alikuwa mtu wa tabaka la matajiri na alikuwa ofisa mwandamizi katika serikali. Alikuwa mwenye elimu nyingi na alikuwa hodari wa mambo ya diplomasia, kwa hiyo alipendwa na kuaminiwa sana na mfalme wa Dola la Chu. Katika kipindi hicho kila mfalme alikuwa anawakusanya watu wenye elimu kwa unyekekevu, na hali hiyo ilishamiri sana katika kila dola. Wasomi wengi wakubwa walitembeatembea kati ya madola ili watimize malengo yao ya kisiasa. Lakini Qu Yuan alikuwa kinyume na hali hiyo, aling’ang’ania kukaa nchini Chu akitumai kumsaidia mfalme wake kwa elimu yake na kumwelimisha mfalme awe fikra za kimaendeleo na kulifanya Dola la Chu liwe la nguvu na ustawi. Lakini bahati mbaya aligongana sana na kundi la matajiri katika mambo ya ndani na nje, na zaidi ya hayo alisingiziwa na wengine, hivyo alipuuzwa na mfalme wa Chu. Tokea hapo hadhi ya Dola la Chu ilishuka na nguvu zilififia. Mwaka 278 K.K. jeshi la Dola la Qin lilivamia Dola la Chu na liliteka mji mkuu wa Dola la Chu. Taifa liliporomoka, na Qu Yuan alijitumbukiza mtoni kutokana na huzuni na hasira.

Maandishi aliyowaachia watu wa baadaye ni utenzi wake Li Sao (uchungu wa moyo). Utenzi huu kwa kutumia mifano ya mambo ya kale alitamani mfalme wa Chu angekuwa kama wafalme werevu wa kale Yao, Shun na Yu waliothamani watu wenye elimu na hekima, na kwa uadilifu na maadili kuendesha utawala na kuunganisha madola mengine kupambana na Dola la Qin.