中国国际广播电台
Katika
Enzi ya Yuan, Guan Hanqing alikuwa
mwandishi mkubwa wa tamthilia.
Tamthilia yake ya kuhuzunisha
“Theluji katika Majira ya Joto”
imechezwa kwa miaka 700 tokea
ilipotungwa, na ilitafsiriwa
kwa lugha nyingi na kuenea duniani.
Guan Hanqing aliishi katika
karne ya 13, Enzi ya Yuan,
alikuwa mtu mwerevu, mcheshi
na mwenye elimu pana. Kadhalika,
alikuwa hodari wa kupiga kinanda,
kucheza ngoma, kupiga filimbi
na kuwinda. Guan Hanqing kwa
miaka mingi aliishi kwenye
mji mkuu na aliwahi kuwa mganga
katika hospitali ya kifalme,
lakini alikuwa hana hamu na
kazi hiyo bali alipenda zaidi
kutunga tamthilia.
Katika miaka aliyoishi,
jamii katika Enzi ya Yuan
ilikuwa ya wasiwasi, na utawala
ulikuwa mbaya, migongano kati
ya matabaka na kati ya makabila
ilikuwa mikubwa, wananchi
waliishi vibaya. Guan Hanqing
aliwahurumia sana watu maskini,
aliacha wadhifa wake alikwenda
miongoni mwa watu maskini
ili kuwaelewa maisha yao na
kwa kutumia tamthilia zake
alifichua ubovu wa jamii na
kuonesha matumaini yake.
Kutokana na kuwa alielewa
sana maisha ya makabwera na
kufahamu lugha zao, alipata
uwezo mkubwa wa kuandika tamthilia
zake. Tamthilia zake ziliwalilia
watu walionyanyaswa na kuonesha
moyo wa kupambana na unyanyasaji
huo.
Tamthilia “Theluji katika
Majira ya Joto” ilieleza uonevu
uliompata msichana Dou E.
Tamthilia hiyo ilipendwa sana
na watazamaji katika karne
kadhaa zilizopita, na inasifiwa
kuwa ni moja ya tamthilia
kumi za kuhuzunisha za China
ya kale.
Maishani mwake Guan Hanqing
aliandika tamthilia 67, lakini
zilizobaki mpaka sasa ziko
18 tu. Katika tamthilia zake
alikuwa makini sana kuumba
taswira ya wahusika na kuonesha
hisia za moyoni. Kati ya waandishi
wa tamthilia hakuna hata mmoja
kama yeye aliyefanikiwa kuumba
sura nyingi mahususi zilizo
tofauti katika tamthilia.
Guan Hanqing anachukua nafasi
muhimu katika historia ya
tamthilia na fasihi ya China,
anasifiwa kama ni “Shakespeare
wa Mashariki”.
|