中国国际广播电台
Mwanzoni
mwa karne ya 18, kitabu maarufu
cha hadithi fupi fupi yaani
“Hadithi za Mashetani” kiliibuka
nchini China, Pu Songling kwa
ustadi wake aliandika hadithi
nyingi za mashetani na bweha.
Pu Songling alizaliwa mwaka
1640 na kufa mwaka 1715, alikuwa
mwanafasihi katika Enzi ya
kifalme ya Qing. Alizaliwa
katika ukoo wa wafanyabiashara,
lakini alifanya kazi ya ualimu.
Katika maisha yake aliandika
makala mengi na kitabu chake
cha mkusanyiko wa hadithi
fupi yaani "Hadithi za
Mashetani" ndicho kilichompatia
umaarufu.
Kitabu cha “Hadithi za Mashetani”
kimekuksanya hadithi 430,
ambapo miongoni mwa hadithi
hizo iliyo fupi kabisa ina
maneno mia mbili au tatu hivi,
na ile ndefu sana ina maelfu
kadhaa ya maneno. Kitabu kizima
kinaeleza hadithi za mashetani
na bweha kikilaani pingu za
maadili ya kimwinyi, ubovu
wa mitihani ya kifalme ya
kuchagua maofisa na kudai
uhuru wa maisha ya binadamu.
Katika kitabu hiki hadithi
za kupendeza sana ni zile
za mapenzi kati ya mashetani
na bweha ambazo zilionesha
matumaini ya binadamu kuvunja
pingu za maadili ya kimwinyi
kati ya wanaume na wanawake.
Katika kitabu cha “Hadithi
za Mashetani” bweha hujitokeza
kama kisura. Miongoni mwa
hadithi hizo, maarufu zaidi
ni “Hadithi ya Xiao Cui”.
Hadithi hiyo iliandikwa kwa
vituko vingi vya kuwavutia
wasomaji, ambapo mwandishi
alimsawiri kwa ustadi msichana
mmoja mwenye akili, roho nzuri
na wa kupendeza. Mwishoni
mwa hadithi hiyo mwandishi
alibainisha kwamba Xiao Cui
alikuwa bweha mdogo, kwa sababu
mama yake aliwahi kukimbia
janga nyumbani kwa wale wazee,
akajigeuza kuwa binadamu ili
kuwalipa wema wao.
Katika kitabu cha "Hadithi
za Mashetani", pia wako
bweha wenye sura mbaya lakini
roho nzuri. Hadithi ya “Bweha
Mwenye Sura Mbaya” ilieleza
jinsi bweha mmoja mwenye sura
ya kuchukiza alivyomkuta msomi
mmoja, ambaye alikuwa maskini
hahehohe hata chakula kilikuwa
ni shida kwake achilia mbali
nguo. Bweha huyo alimsaidia
maisha yake. Lakini baada
ya msomi huyo kupata nguo
safi, nyumba za fahari na
kila kitu kwa maisha ya starehe
alimwomba mchawi amfukuze
bweha. Bweha alihamaki sana
kutokana na msomi huyo kukosa
shukrani, ndipo licha ya kurudisha
yote aliyompa msomi, alimtuma
shetani kumwadhibu vibaya.
Kwa masimulizi ya hadithi
hii mwandishi anawaonya watu
wenye roho mbaya.
Katika kitabu cha "Hadithi
za Mashetani" mwandishi
Pu Songling pia alitunga hadithi
ya bweha kisura lakini mwenye
roho katili. Hadithi ya "Kuchora
Ngozi ya Mrembo" ilieleza
kuwa bweha mmoja alijifunika
kwa ngozi yenye sura nzuri
akiishi kwa kufyonza damu
za binadamu, bweha huyo mwishowe
aliuawa na binadamu.
Kwa kifupi, Pu Songling
aliwaelezea wasichana wengi
kwa sura ya bweha, na wasichana
hao walikuwa na maadili mengi
mazuri ambayo binadamu hawakuwa
nayo.
"Hadithi za Mashetani"
ni maandishi makubwa katika
historia ya fasihi ya Kichina.
Katika miaka mia mbili iliyopita
hadithi hiyo imetafsiriwa
kwa lugha zaidi ya 20, na
hadithi nyingi zilitengenezwa
kuwa filamu na michezo ya
televisheni.
|