"Safari ya Kwenda Magharibi" 
中国国际广播电台

      
"Safari ya Kwenda Magharibi" ni riwaya nzuri katika historia ya fasihi ya kale ya China. Riwaya hii ilitungwa kwa mujibu wa vituko vilivyomkuta sufii wa dini ya Kibuddha, Tang Zeng (Tang Xuanzang), alipokuwa katika safari yake ya kwenda India kuchukua msahafu katika karne ya 7 K.K. Katika riwaya hiyo Wu Chengen alibuni wafuasi watatu kufuatana na sufii huyo. Mmoja wa wafuasi wake alikuwa mfalme kima Sun Wukong. Sun Wukong alikuwa na nguvu za kudura ya mungu, anaweza kujigeuza sura 72 na fimbo yake ya kupambana na mashetani yaweza kurefushwa kuwa ndefu hadi mbinguni na kufupishwa kuwa ndogo hadi kama sindano ya kutia sikioni. Mfalme kima Sun Wukong ndiye aliyeonesha matumaini ya mwandishi kwamba mambo yote maovu yatatokomezwa kabisa katika jamii.

Wu Chengen ni mwenyeji wa wilaya ya Huai An mkoani Jiangsu. Tangu alipokuwa mtoto alikuwa mwerevu na mshabiki wa mambo mengi. Alikuwa hodari wa kuchora picha, usanii wa maandiko ya Kichina kwa brashi ya wino, pia alipenda kukusanya na kuhifadhi picha na maandiko ya watu mashuhuri. Alipokuwa kijana jina lake lilikuwa maarufu sana katika sehemu ya makazi yake kwa sababu ya kipaji chake cha fasihi. Lakini mara nyingi alishindwa katika mitihani ya kifalme ya kuchagua maafisa, na maisha yake yakawa ya shida. Kutokana na hayo akagundua ubovu ulioenea miongoni mwa maafisa na jinsi jamii ilivyotatanika, akawa na kinyongo moyoni mwake. Katika shairi lake moja alisema kwamba ubovu wa jamii unatokana na mfalme kuwatumia maafisa wabovu. Alitaka kubadilisha hali hiyo lakini hakuweza kufanya lolote ila kuipigia kite. Hivyo aliweka matumaini na kinyongo chake kwenye riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi".

"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa na Wu Chengen katika miaka yake ya uzeeni, lakini matayarisho ya riwaya hiyo yalimtumia maisha yake yote. Alipokuwa mtoto mara kwa mara alifuatana na baba yake kwenda kwenye misitu minene na mahekalu, na baba yake humweleza hadithi za ajabu zilizotokea huko. Hamu yake ya kusikiliza hadithi utotoni mwake haikupungua hata baada ya yeye kuwa mzima. Baada ya kutimiza miaka 30 alikuwa amekusanya hadithi nyingi za ajabu akanuia kuandika riwaya. Alipofikia umri wa miaka 50 hivi alikuwa amemaliza sura 10 za mwanzo za riwaya yake ya "Safari ya Kwenda Magharibi", lakini baadaye kwa sababu fulani aliacha kwa miaka mingi hadi baada ya kujiuzulu kazi na kuwa nyumbani.

"Safari ya Kwenda Magharibi" iliandikwa hadithi moja moja lakini kila hadithi pia ni sehemu ya riwaya nzima. Ndani ya riwaya hiyo walitokea mashetani na miungu mingi ambao wanawakilisha haki na uovu. Kasri ya mbinguni ilionekana adhama sana lakini kwa kweli mungu aliyekuweko ndani ya kasri hiyo alikuwa mbabaishaji wa watu wema na wabaya, akilenga mfalme duniani; na kasri ya dunia ya pili ingawa ilionekana ukakamavu, lakini maofisa wanasaidiana katika hatia, walikuwa hawajali sheria na wadhulumiwa hawakuweza kupata haki. Hayo alilenga katika hali ya utawala wa kifalme. Mashetani walikula na kuwaua watu huku wakiwa wachoyo wa mali na kupenda warembo na kufanya uovu watakavyo. Katika hayo mwandishi alifananisha madhalimu na maofisa wa kifalme. Kwa upande mwingine Wu Chengen alifanikiwa kusawiri shujaa kima Sun Wukong, ambaye alikuwa mtetezi wa haki, alikuwa na nguvu za kudura ya mungu na mwenye msimamo bayana kati ya watu wema na wabaya, fimbo yake ina nguvu za ajabu. Hii inaonesha tarajio la Wu Chengen la kukomesha maovu yote katika jamii aliyoishi.

Riwaya ya "Safari ya Kwenda Magharibi" inajulikana sana kwa wote wa China kutoka kizazi hadi kizazi na katika miaka mia kadhaa iliyopita riwaya hii ni kama chimbuko la kutunga hadithi kwa watoto na michezo ya filamu na televisheni.