"Utenzi wa Mfalme Gesar"
中国国际广播电台

      
Utenzi wa Mfalme Gesar ni utenzi wa kale na mrefu kabisa duniani, na mpaka sasa unaimbwa kumsifu mfalme shujaa Gesar katika Tibet.

Utenzi wa Mfalme Gesar ulipatikana tokea miaka mia mbili K.K. hadi karne ya sita kutoka masimulizi ya mapokeo, na ifikapo karne ya 12 utenzi huo ulikuwa umekamilika, na kuenea mpaka sasa mkoani Tibet.

Utenzi wa Mfalme Gesar unasimulia hadithi kama ifuatayo: Katika zama za kale, maafa makubwa yalitokea katika Tibet, licha ya maafa ya kimaumbile pia mashetani walifanya uovu na kuwanyanyasa watu kiholela. Mungu mdogo wa kike mwenye huruma Pu Sa alimwomba Buddha awapeleke askari wake kushuka duniani kuwaangamiza mashetani. Buddha alimteua Gesar awe mfalme na kupambana na mashetani na awaletee maisha bora watu wa Tibet. Watungaji wa utenzi huo walitunga shujaa mwenye nusu binadamu na nusu mungu. Gesar alikuwa hatarini mara kadhaa lakini kutokana na ulinzi wa mungu kila mara alisalimika, na aliwaua mashetani wengi. Tokea alipozaliwa Gesar alianza kuwaokoa watu kutoka kwenye misiba mingi. Alipokuwa na umri wa miaka 12 alishinda katika mashindano ya mbio za farasi na alichaguliwa kuwa mfalme. Tokea hapo alianza kuonesha ushupavu wake wa kupambana na mashetani huku na huko na kuwaua mashetani wengi. Mchango wake ulikuwa ni mkubwa na baada ya kumaliza jukumu lake duniani alirudi mbinguni.

Utenzi wa Gesar ni mrefu, una beti zaidi ya milioni moja wenye maneno milioni 20 katika juzuu 120, ni utenzi mrefu kabisa duniani.