Hadithi ya “Kupekecha Moto”

中国国际广播电台


    Zamani za kale, binadamu walikuwa hawakujua maana ya moto wala matumizi yake. Usiku ulipoingia, giza totoro lilifunika kila mahali, wanyama walikuwa wakinguruma huku na huko, watu wakijikunyata kwa hofu na baridi. Kwa sababu ya kutokuweko moto, iliwalazimu binadamu kula vyakula visivyopikwa, kwa hiyo mara kwa mara waliugua na umri wao wa kuishi ulikuwa mfupi.

Mbinguni alikukwako mungu mmoja mkubwa ambaye alijulikana kama Fu Yi. Alipoona jinsi maisha yalivyowawia vigumu binadamu, aliwahurumia sana, alitaka kuwafahamisha namna ya kutumia moto. Fu Yi kwa kudra yake alinyesha mvua kubwa ya radi kwenye msitu. Ka! Sauti kali ya kupasua masikio ilizagaa angani, papo hapo radi ilipiga na mti ukawaka, moto uliongezeka kuwa mkubwa. Watu walitishika vibaya, walikimbia ovyo. Muda si muda mvua ilisimama, usiku ulianguka, baridi ilikuwa kali zaidi baada ya mvua. Waliokimbia walirudi wakakusanyika pamoja wakiangalia moto ulivyowaka kwa nguvu. Wakati huo kijana mmoja alitanabahi kuwa hapo kabla wanyama walionekana huku na huko lakini sasa wametoweka kabisa, akafikiri, “Kwani wanyama wanaogopa kitu hiki kinachong'ara?” Kwa ujasiri akausogelea moto, akasikia joto, kwa furaha akawaita wenzake kwa kelele, “Ebu, njooni haraka, moto huu si kitu cha kuogopwa, kinatupatia joto na mwanga!” Wakati huo watu wengine waligundua wanyama walioungua kwa moto, harufu nzuri ya nyama iliyochomwa ilipenya puani. Watu walikusanyika karibu na moto, waligawana nyama, utamu wa chakula ambao hawakuwahi kuuonja uliwashangaza kweli, waliona moto ni kitu kizuri sana, hivyo wakaokota matawi ya miti wakayawasha na kila siku walipokezana kwa zamu kuuhifadhi moto huu ili usizimike. Lakini kwa bahati mbaya, siku moja mwenye zamu alipitiwa na usingizi, kuni zilikwisha na moto ukazimika. Watu wakaingia tena katika hali ya giza na baridi, maisha yakawaletea matatizo makubwa.

Mungu Fu Yi aliyaona yote yaliyowatokea, alijitokeza katika ndoto ya yule kijana aliyegundua moto, akamwambia, “Kutoka hapa upande wa magharibi, iko nchi moja inayoitwa Sui Ming Guo, huko utapata moto, nenda ukachukue moto na kuleta hapa.” Kijana huyo alizinduka kutoka usingizini, alikumbuka wazi maneno aliyoambiwa ndotoni akashika njia ya kwenda kutafuta ule moto.

Kijana huyo alisafiri mbali, alipita milima, mito na misitu, alipata shida kubwa safarini, mwishowe alifika ile nchi ya Sui Ming Guo. Lakini huko hapakuwa na mwanga wa jua, bali giza liligubika kila mahali. Kuona hali hiyo kijana alikata tamaa, akajitupa kwenye mti mmoja kutweta kwa sababu ya uchovu. Ghafla mwanga ulimulika, aliona ndege kadhaa wakubwa wakubwa wakidonoa wadudu kwa midomo yao mifupi na migumu kwenye gogo la mti, kila walipogogota mwangaza hutatarika, lakini moto haukuwaka. Kuona jinsi cheche za moto zilivyotokea kichwa kilimduru, kisha kijana akatumia vijiti vidogo akijaribu kupekecha kwenye vijiti vinene, cheche zilitoka, lakini pia moto haukuwaka. Kijana hakukata tamaa, alijaribu kwa vijiti hivi na vile vya miti tofauti, mwishowe moshi ukaanza kufuka punde si punde moto ukawaka. Oo! Kijana akafurahi kweli kiasi cha kutokwa na machozi.

Kijana alirudi nyumbani, aliwaletea wenyeji ujuzi wa namna ya kupata moto, njia ya kupekecha. Tokea hapo binadamu wameachana na maisha yasiyo na nuru. Kutokana na uwerevu na ushupavu wake, binadamu wakamwita kijana huyo “Sui Ren”, maana yake ni mtu aletaye moto.