Jinsi Wafalme wa Kale Walivyong'atuka katika China

中国国际广播电台

Katika historia ndefu ya jamii ya umwinyi nchini China wafalme waliwarithisha watoto wao wa kiume viti vya enzi, lakini katika China ya kale, wafalme wa mwanzoni kabisa Yao na Shu hawakufanya hivyo bali waliwaachia viti vyao watu wasio na uhusiano wa kidamu. Yeyote aliyekuwa na maadili na uwezo alipendekezwa kuwa mrithi. Katika kipindi hiki nimewaletea masimulizi ya hadithi ya mfalme Yao jinsi alivyomrithisha enzi yake Shun.

Yao alikuwa mfalme wa kwanza katika China, alipozeeka alitaka kuchagua mrithi wake, siku moja aliwakusanya watemi wote kujadili mrithi wake.

Baada ya Yao kuelezea nia yake, mmoja wa watemi aitwaye Fang Qi alisema, “Mwanao Zhu Dan ni mtu mwenye fikra za kimaendeleo, anafaa kuwa mrithi wako.” Kusikia hayo mfalme Yao alisema, “Hapana, huyo hana maadili mema, ana tabia ya kuzozana na watu.” Kisha mwingine alisema, “Diwani anayesimamia hifadhi ya maji Gong Gong labda anafaa.” Mfalme Yao alitikisa kichwa akisema, “Huyo ni hodari wa kuongea tu, mbele yako anakufurahisha kwa kukusifu lakini ana mengine moyoni mwake, sina imani naye.” Majadiliano hayakuwa na matokeo, Yao aliendelea na kiti chake cha ufalme, lakini hakuacha kuendelea kutafuta mrithi wake.

Baada ya kipindi kirefu kupita, mfalme Yao aliwakusanya tena watemi kujadilia urithi wake. Kwenye majadiliano watemi kadhaa kwa kauli moja walimpendekeza kijana mmoja kabwela, Shun. Mfalme Yao aliinamisha kichwa na kusema, “Ndio, pia nimesikia habari zake, hebu nifahamishe zaidi jinsi alivyo?” Watemi waliongea mengi juu yake: Baba yake alikuwa mjinga wa mwisho, watu humwita mzee kipofu. Mama yake mzazi keshakufa zamani, mama yake wa kambo alimtendea vibaya Shun baada ya kumzaa mtoto wake Xiang. Xiang ni mtu mwenye kiburi, lakini mzee kipofu alimdekeza kupita kiasi. Ingawa Shun anaishi katika familia kama hiyo anawatendea vema baba na mama yake wa kambo na ndugu yake Xiang, hivyo majirani wanamsifu kwa maadili yake.

Baada ya kusikiliza maelezo yao, Yao alitaka kuhakikisha kwa kumpima zaidi. Aliwaozesha binti zake wawili E Huang na Nu Ying kwa Shun, akampatia ghala ya nafaka, akamgawia ng'ombe na mbuzi wengi. Mama yake wa kambo na ndugu yake Xiang walipoona mali hizi waliona husuda na wivu, basi wakishirikiana na baba yake walikula njama ya kumwua.

Siku moja baba yake alimwambia Shun atie kirago paa la ghala ya nafaka. Baada ya Shun kupanda paa baba yake aliwasha moto chini akitaka kumwunguza kwa moto. Shun alitaka kushuka haraka kwa ngazi, lakini ngazi ilikuwa imeondolewa, kwa bahati alivaa kofia kubwa ya ukili, aliitumia na kuruka chini kama parachuti, akaanguka bila kuumia.

Baba na ndugu yake Xiang hawakufa moyo, baadaye walimwambia Shun ashuke kisimani kuondoa matope, lakini aliposhuka tu baba yake na ndugu yake walitupa mawe wakitaka kumzika mule ndani, lakini hawakujua kuwa Shun angechimba pango pembeni akajipenyeza nje bila kuumia hata kidogo.

Xiang na baba yake walirudi nyumbani kwa furaha bila kujua kwamba Shun alikuwa amesalimika. Xiang alisema “Leo tumemfikisha kaka yangu ahera, ujanja huu ni mimi nilioubuni. Haya, sasa tugawane mali zake.” Kisha akaendea chumba cha kaka yake, lakini alipoingia chumbani alimwona kaka yake akicheza kinanda kitandani. Alishituka, lakini baada ya kutuliza moto kwa haya alisema, “Ah, kaka yangu mpenzi nakukumbuka sana.”

Shun alijitia hamnazo, akasema, “umekuja wakati mzuri, shughuli zangu ni nyingi naomba unisaidie.” Shun aliendelea kuwatendea vema baba na mama yake wa kambo na ndugu yake. Tokea hapo baba na ndugu yake hawakuthubutu tena kumwua kwa hila.

Baadaye mfalme Yao aliendelea kumpima kwa mambo mengi, akabainika kuwa Shun kweli ni mtu mwenye maadili na uwezo mkubwa, akaamua kumwachia kiti cha enzi yake.

Baada ya Shun kuwa mfalme, maisha yake yalikuwa kama ya raia, hakuacha kazi za mikono, akapata imani na heshima ya raia wake. Baada ya miaka kadhaa Yao alifariki, wakati huo Shun alitaka kumtawaza mtoto wa Yao, Zhu Dan, lakini watemi hawakukubali. Shun alipozeeka alitumia njia hiyo hiyo kuchagua mrithi wake Yu kwa maadili na uwezo. Lakini Yu alipozeeka alimwachia kiti chake cha ufalme mtoto wake wa kiume Qi. Tokea hapo kiti cha ufalme kikawa kinarithiwa na mtoto wa kiume wa mfalme kizazi hadi kizadi katika jamii ya umwinyi yenye historia ya miaka elfu kadha nchini China.

Katika enzi za Yao, Shun na Yu jamii ilikuwa tulivu bila ya mapambano ya kuwania maslahi ya kibinafsi wala madaraka ya utawala, wafalme walikuwa sawa na raia wakiishi maisha ya kawaida.