Hadithi kuhusu Milima Mitano ya Ajabu

中国国际广播电台


Baada ya malaika Nu Wa kuumba binadamu (hadithi yake tuliwahi kueleza katika kipindi kilichopita), dunia ilikuwa na utulivu kwa kipindi kirefu. Lakini siku moja ghafla mbingu na ardhi ziligongana kwa nguvu, mbingu ikapasuka na ardhi ikadidimia huku moto mkubwa ukitoka ardhini na kunguza misitu; mafuriko makubwa ya maji yaliporomosha milima, mashetani, vibwengo na wanyama wakali walitumia nafasi hii kufanya mambo maovu watakavyo, binadamu walizama kwenye bahari ya misiba.

Nu Wa alisikia kilio cha binadamu, kwanza aliwaua wale mashetani na vibwengo na wanyama wote wabaya, kisha akatuliza maji, baada ya yote hayo kufanyika alianza kazi yake kubwa ya kuziba ufa uliotokea mbinguni.

Nu Wa alikusanya majani na kuni na kurundika rundo kubwa kiasi cha kufikia mbinguni, kisha akatafuta mawe yaliyokuwa na rangi ya samawati sawa na ya mbingu, lakini kwa kuwa duniani hakukuwepo mawe hayo mengi aliyotaka, hivyo ilimpasa akusanye mawe mengine meupe, njano, mekundu na meusi na kuyaweka juu ya lile rundo. Alichukua moto uliokuwa karibu kuzimika akawasha mti mmoja mkubwa na kuwasha rundo lake la majani. Moto uliwaka zaidi na zaidi ukaangaza ulimwengu mzima, na mawe yenye rangi tano yalichomwa yakawa mekundu. Baada ya muda yakaanza kuyenyuka na kuwa kama uji ambao ulitiririka na ukaziba ule ufa wa mbingu. Baadaye moto kwenye rundo ulizimika, na ufa ukawa umezibika tayari.

Ingawa mbingu ilikuwa imekamilika lakini haikuwa kama ya awali. Sehemu ya kaskazini-magharibi iliinama kidogo, kwa hiyo jua na mwezi huendea huko; ardhi, sehemu ya kusini-mashariki ilididimia, kwa hiyo mito na vijito hutiririkia huko, maji yaliyokusanyika huko miaka nenda miaka rudi yakawa bahari.

Katika upande wa mashariki ya bahari lilikuwako bonde moja kubwa ambalo kina chake kilikuwa kirefu kiasi cha kutoweza kuona mwisho wake. Bonde hilo linajulikana kama Gui Xu na maji ya mito na ya bahari yanaingia kwenye bonde hilo, lakini kiwango cha maji ni kile kile wala hakiongezeki kuwa mafuriko kiasi cha kuwaletea watu maafa.

Ndani ya bonde la Gui Xu kuna milima mitano ya ajabu, nayo ni Dai Yu, Yuan Qiao, Fang Hu, Ying Zhou na Peng Lai. Kila mmoja ulikuwa na urefu wa kilomita elfu kumi na ulitengana kwa kilomita elfu ishirini. Mlimani kuna kasri iliyojengwa kwa dhahabu na marumaru ambako miungu mingi waliishi.

Mlimani, ndege wote walikuwa weupe, miti ilikuwa mingi na ya ajabu, matunda ya miti hiyo yalikuwa kama lulu na vito, ladha tamu sana, watu wa kawaida wakila wataishi milele bila kuzeeka. Miungu walivaa mavazi meupe pia na wana mabawa madogo meupe mgongoni, waliruka huku na huko kati ya milima kuwatembelea marafiki na jamaa zao chini ya mbingu iliyotakata, maisha yao yalikuwa ya furaha bila kifani.

Hata hivyo, furaha yao haikuwa imekamilika. Sababu ni kuwa milima hiyo mitano haikuwa na mizizi bali ilielea baharini, kwa hiyo upepo mkubwa ukivuma milima hiyo huenda mrama na kuelea bila ya kutulia sehemu maalumu. Hali hiyo ilitia doa katika furaha yao. Kwa hiyo miungu walichagua mjumbe mmoja kwenda peponi kueleza usumbufu huo. Baada ya kufahamishwa, mungu wa peponi pia alipata wasiwasi kwamba milima hiyo mitano ingeelea mbali na kutoweka, miungu hiyo wangepoteza maskani yao, basi akaamrisha mungu wa bahari “Yu Qiang” atume kasa wakubwa kumi na tano waende huko kubeba milima hiyo mitano mgongoni.

Kila mlima ulibebwa na kasa mmoja huku wengine wawili wakisubiri zamu yao ambapo watabadilishana kila baada ya miaka elfu sitini. Kwa kufanya hivyo milima ikatulia tuli, miungu yote milimani wakaingiwa na furaha.

Bila kutegemewa, mwaka fulani, jitu moja kutoka “Dola ya Majitu” alikuja kwenye bonde la Gui Xu kuvua samaki kwa mshipi, mwili wake ulikuwa mkubwa kama mlima. Muda si mrefu alivua kasa sita waliokuwa wamebeba milima miwili. Lakini jitu hakuwa na habari, alibeba kasa hao mgongoni akarudi nyumbani. Milima hiyo miwili, Dai Yu na Yuan Qiao, bila ya kubebwa na kasa ilielea elea hadi nchi ya kaskazini ya dunia kwa kusukumwa na upepo na kuzama huko baharini. Miungu walioishi katika milima hiyo miwili waliruka ruka angani kwa mahangaiko wakiwa na mali zao na kulowa na majasho.

Kusikia habari hiyo mungu wa mbinguni akacharuka, mara akamfupisha yule jitu wa “Dola ya Majitu” asije akaleta matata mengine. Milima mitatu iliyobaki ilikuwa salama kwa kuwa inaendelea kubebwa na kasa mpaka leo kwenye ufukwe wa mashariki ya China.