Pan Gu Aumba Mbingu na Ardhi

中国国际广播电台


     Kama tujuavyo, kila taifa lina hadithi nyingi za mapokeo, visasili na aina nyingi nyingine, hadithi hizo ni msingi mojawapo wa utamaduni wa taifa. Leo basi, katika kipindi hiki nimewaletea hadithi moja ya kubuniwa, ijulikanayo kama “Pan Gu Aumba Mbingu na Ardhi”.

Inasemekana kwamba zamani za kale ulimwengu ulikuwa kama yai kubwa, na ndani yake yalikuwa machafuko matupu, giza totoro, kulikuwa hakuna juu wala chini, hakuna mashariki, magharibi wala kaskazini na kusini. Lakini ndani yake lilimlea shujaa mmoja aliyeumba mbingu na ardhi: Pan Gu. Pan Gu alilelewa ndani ya yai hilo kwa miaka elfu kumi na nane, mwishowe alizinduka kutoka usingizini. Alifumbua macho lakini hakuweza kuona chochote kwa ajili ya giza tupu, alikuwa hawezi kuvumilia kwa sababu ya joto kali mule ndani, alitaka kusimama lakini alibanwa na gamba la yai hata asiweze kunyoosha miguu. Kutokana na hali hiyo ngumu Pan Gu alikasirika, akachukua shoka alilozaliwa nalo, akalivumisha kwa nguvu, sauti kali ikarindima, yai likapasuka. Yale yaliyokuwa mepesi na safi ndani ya yai hilo yakaelea juu na juu kukawa mbingu na yale yaliyokuwa mazito na machafu yakazama chini na chini kukawa ardhi.

Pan Gu alifurahi mno kwa kufanikiwa kuumba mbingu na ardhi, lakini alihofia mbingu na ardhi zingeungana baadaye. Basi akatumia kichwa kuhimili mbingu na kutumia miguu kukanyaga ardhi huku akionyesha uwezo wake wa ajabu: Kila siku alikua kimo cha mita tatu, hivyo mbingu ikawa juu mita tatu, na ardhi ikaongeza maki mita tatu. Vivyo hivyo muda ukapita miaka elfu kumi na nane. Pan Gu akawa pandikizi la mtu ambaye kichwa chake kiligusa mbingu na miguu yake ilikanyaga ardhi, kimo chake kilikuwa kilomita elfu 500. Haijulikani kama maelfu mangapi ya miaka yalipita, mbingu na ardhi ikatulia tuli bila ya kuweza kuungana pamoja, wakati huo ndipo Pan Gu alitulia moyo, lakini alikuwa amechoka sana, akafa.

Baada ya Pan Gu kufariki, maiti yake ilibadilika kiajabu: Jicho lake la kushoto likawa jua jekundu, la kulia likawa mwezi, pumzi yake ya mwisho ikawa upepo na mawingu, sauti yake ya mwisho ikawa mngurumo wa radi, nywele na ndevu zake zikawa nyota, kichwa, mikono na miguu yake ikawa milima, damu yake ikawa mito na maziwa, mishipa ikawa njia, misuli ikawa ardhi yenye rutuba, ngozi na malaika yakawa mimea na miti, meno na mifupa ikawa madini na jasho lake likawa mvua na umande. Kuanzia hapo ikatokea dunia.

Hapo awali baada ya Pan Gu kuumba mbingu na ardhi, humu duniani hapakuwa na binadamu. Siku moja malaika mmoja ajulikanaye kama Nu Wa alishuka duniani, aliona dunia ilikuwa na kimya bila uchangamfu wa viumbehai. Alikwenda kwenye ukingo wa mto akachota maji kwa mikono kutaka kunywa, wakati huo akaona sura yake majini, mara akatumia udongo na maji kufinyanga finyanga sanamu kwa mujibu wa sura yake, kisha akaipuliza sanamu na sanamu ikawa mtoto wa kike, aliendelea kufinyanga sanamu nyingine na ikawa mwenzi wa mtoto wa kike, na huyo alikuwa mwanamume wa kwanza duniani. Malaika Nu Wa alifurahi sana, basi akaanza kufinyanga finyanga akitaka binadamu wajae duniani. Lakini dunia ni kubwa mno hakuweza kutimiza nia yake kwa muda mfupi. Wakati huo huo akapata ujanja, akachukua tawi la mti na kulitia mtoni kukorogakoroga, matope yakanasa kwenye tawi la mti, kisha akalikung'uta, matone ya matope yakasambaa ardhini na yakawa watu wadogo wadogo, wanaume na wanawake wakichanganyikana. Muda si muda dunia ikajaa binadamu. Lakini tatizo lingine likatokea, Nu Wa alifikiri, watu hao mwishowe watakufa, itampasa afinyange tena, kazi ya ufinyanzi itamsumbua. Kufikiri hivyo aliwaita watu wote mbele yake, akawaambia wazaliane wenyewe, basi binadamu wakaanza kubeba jukumu la kuzaa. Tokea hapo binadamu wakawa wanazaliana kizazi baada ya kizazi.