Hadithi ya Kabwela Niu Lang na Malaika Zhi Nu

中国国际广播电台


      Niu Lang alikuwa mseja maskini, aliishi kwa kumtegemea tu ng'ombe mmoja na plau moja. Kila siku Niu Lang alitoka nyumbani alfajiri mapema kwenda kulima shambani na kurudi machweo akiwa hoi; aidha ilimpasa ajifulie nguo na kujipikia chakula. Maisha yalimwia vigumu sana. Lakini siku moja alitokewa na miujiza.

Kutokana na uchovu, Niu Lang alijikokota hadi nyumbani baada ya kazi ngumu shambani. Alipoingia chumbani alipatwa na mshangao: Chumba kilikuwa safi sana, nguo zilikuwa zimefuliwa tayari, chakula kitamu kilikuwa mezani kikiwa bado moto moto. Niu Lang alikodolea macho yote hayo, akiwaza: Vipi mambo haya? Kwani malaika ameshuka kutoka mbinguni?

Tokea hapo, hali ilikuwa vivyo hivyo katika siku kadhaa mfululizo. Niu Lang alitaka kujua sababu yenyewe. Basi siku moja, kama kawaida yake alitoka nyumbani mapema, lakini hakwenda shambani, bali alijificha sehemu jirani na nyumbani huku akikaza macho kuvizia.

Muda si muda alikuja msichana mmoja mrembo, akaanza kushughulika baada ya kuingia chumbani. Wakati huo Niu Lang alishindwa kujizuia, akakimbilia chumbani na kusimama mbele yake, akamwuliza: “Ewe msichana kwa nini umekuja nyumbani kwangu kunishughulikia?” Kusikia sauti hiyo msichana alishituka, akajibu kwa sauti ndogo kama ya mnong'ono huku uso ukiwa umemwiva: “Naitwa Zhi Nu, naona umepata shida sana katika maisha yako, nimekuja kukusaidia.” Niu Lang akafurahi sana, akajikakamua na kusema, “Tuoane basi, tuishi na kufanya kazi pamoja.” Zhi Nu akakubali. Niu Lang na Zhi Nu wakafunga pingu za maisha. Niu Lang alikwenda kulima kila siku na Zhi Nu alishughulika na kazi za nyumbani na kufuma nguo. Maisha yalikuwa ya kufurahisha.

Baada ya miaka kadhaa kupita, walijaliwa watoto wawili, wa kiume na wa kike, na hivyo furaha ilitawala familia hiyo.

Lakini siku moja ghafla mawingu mazito yalitanda mbinguni, kimbunga kilivuma kwa nguvu, na askari wawili wa mbinguni wakashuka kwenye nyumba. Niu Lang akaambiwa kwamba Zhi Nu alikuwa mjukuu wa mungu, amekuwa akitafutwa kwa miaka kadhaa iliyopita. Askari walimrudisha Zhi Nu mbinguni kwa nguvu.

Niu Lang akiwa na watoto wawili kifuani alibaki kumwangalia mkewe akichukuliwa na askari wawili kurudi mbinguni, alihuzunika sana, lakini aliapa kwamba atakwenda mbinguni kumchukua mkewe Zhi Nu ili kukamilisha familia yake. Lakini binadamu atawezaje kufika mbinguni?

Niu Lang alipoishiwa na ujanja, ng'ombe wake mzee alimwambia, “Nichinje mimi na kujifunika ngozi yangu mgongoni; kwa namna hiyo utaweza kuruka kwenda mbinguni.” Niu Lang kamwe hakukubali, lakini ng'ombe aling'ang'ania. Kwa kuona hana njia nyingine Niu Lang alimchinja huku akilia.

Niu Lang alijifunika kwa ngozi ya ng'ombe, akawabeba watoto wawili kwa mzegazega, mmoja mbele, mmoja nyuma, akaruka kwenda mbinguni. Lakini huko kwenye kasri ya mbinguni watu waligawanyika kwa matabaka, hakuna yeyote aliyemheshimu kabwela maskini na hohe hahe kama Niu Lang. Mungu alimkatalia ombi lake la kuonana na mkewe Zhi Nu.

Niu Lang na watoto wake walimsihi sana, mwishowe aliruhusiwa kumwona mkewe kwa muda mfupi. Mkewe Zhi Nu aliyekuwa amefungwa alipowaona mumewe na watoto wake alijawa na furaha na huzuni. Kufumba na kufumbua muda ukapita, mungu akaamuru kuondolewa kwa Zhi Nu. Maskini Niu Lang na watoto wake walimkimbilia kadri wawezavyo huku wakianguka anguka na kuinuka. Mwishowe walipomkaribia, mke wa mungu alichomoa kibanio cha nywele akachora mstari angani, na mara mto wa kilimia ukatokea kati yao. Tokea hapo Niu Lang na Zhi Nu wakawa wametenganishwa na mto huo, isipokuwa tu kila tarehe 7 ya mwezi wa 7 wanaruhusiwa kukutana. Kila wakati siku hiyo ilipowadia, ndege wasio na idadi waliungana pamoja na kuwa kama daraja juu ya mto huo ili Niu Lang na Zhi Nu wakutane.