Kua Fu Afuata Jua

中国国际广播电台


     Zamani za kale, katika sehemu ya kaskazini kulikuwako mlima mmoja mrefu uliofikia hadi mawinguni, na huko mlimani kwenye msitu mnene, liliishi kundi kubwa la majitu, ambapo mtemi wao alijulikana kama Kua Fu alikuwa na nyoka mmoja kwenye kila sikioni na wengine wawili mikononi. Kutokana na jina lake pia kabila lake lilijulikana kama kabila la Wakuafu. Watu wa kabila la Wakuafu walikuwa na roho nzuri, wenye bidii za kazi na waliishi kwa amani na utulivu.

Mwaka fulani hali ya hewa ilikuwa joto sana, jua la utosini liliwaka na ardhi ilikuwa joto kiasi cha miti kuungua na mito yote kukauka. Watu wengi walikufa kutokana na joto. Mtemi Kua Fu alihuzunika sana, na siku moja akawaambia watu wake huku akiangalia jua, “Jua hili ni baya sana! Ni lazima nilifuate na kuliamrisha.” Watu wake waliposikia kauli hiyo baadhi walimwasa “Halahala usiende, jua liko mbali sana nasi, utakufa kutokana na safari ndefu.” Wengine walisema “Jua lina moto mkali, utakaushwa kabla ya kulifikia.” Lakini Kua Fu hakuwasikiliza. Aliwaambia watu wake waliokuwa wakisononeka sana, “Ili mweze kupata raha na utulivu wa maisha, ninapaswa kulifuata!”

Kua Fu alianza safari yake baada ya kuagana na watu wake. Alipiga hatua kubwa kubwa na kwa haraka kama upepo. Alipita kwenye milima na milima, mito na mito, huku vishindo vya miguu vilitetemesha ardhi. Katika safarini yake mchanga aliokung'uta kutoka kwenye viatu vyaake ulibadilika kuwa mlima. Mafiga matatu ya kujinjika sufuria alipokuwa akipika chakula yalibadilika kuwa milima mirefu mitatu iliyochongoka.

Kua Fu aliendelea kufuata jua, huku akilikaribia zaidi na zaidi, na hivyo kuwa na imani. Alihisi joto kali zaidi na zaidi, na mwishowe alifikia kwenye sehemu jua lilipozama. Jua lililokuwa kama tufe jekundu la moto lilitoa miali inayouumiza macho. Kua Fu alifurahi sana kiasi cha kutaka kulikumbatia kifuani, lakini kutokana na joto hakuweza, aliona kiu kali na uchofu mkubwa. Alikimbilia kwenye mto Huang He huku akigugumia na kumaliza maji yote, kisha akakimbilia kwenye mto Wei He, akayamaliza tena maji yote ya mtoni, lakini hakukata kiu basi akakimbilia kwenye ziwa kubwa lililoko kwenye sehemu ya kaskazini, lakini akafa kwa kiu kabla hakulifikia.

Kabla ya kufa alisikitika sana alipowakumbuka watu wake jinsi walivyosononeka. Alitupa mkongojo wake, na pale ulipoangukia pakawa msitu mkubwa. Msitu huo uliwaleta mazingira mazuri ya kuishi yenye ubaridi yasiyo na miali mikali ya jua ambapo wasafiri hupumzika huko wakati wakiwa safarini.

“Kua Fu Afuata Jua” ni hadithi inayoonyesha watu wa kale walivyotamani kupambana na kiangazi. Ingawa Kua Fu alikufa lakini moyo wake wa kuwaondolea watu usumbufu na kuwaletea hali nzuri ya maisha utaishi daima. Katika vitabu vyingi vya siku za kale, yako makala mengi kuhusu hadithi hiyo, pia upo mlima wa kumbukumbu uliopewa jina la “Mlima wa Kua Fu”.