Chang E Arukia Mwezini

中国国际广播电台

Tarehe 15 mwezi Agosti kwa kalenda ya Kichina ni sikukuu ya mwezi. Sikukuu hiyo ni mila ya Wachina yenye historia ndefu. Katika siku hiyo jamaa wa familia moja hujikusanya pamoja kula keki za mwezi na kuburudika na mwezi mpevu. Sikukuu hiyo ilitokana na hadithi ya “Chang E Arukia Mwezini”.

Chang E alikuwa mungu wa mwezi, mume wake Houyi alikuwa hodari wa kupiga mishale. Mwaka mmoja duniani ulitokea msiba mkubwa duniani, wanyama wakali walitoka majini na misituni kuwashambulia binadamu. Mungu mkuu alipofahamu hali hiyo alimtuma Houyi ashuke duniani akiwa na mkewe Chang E. Aliwaua wanyama wakali lakini wakati huo mbinguni kulitokea majua kumi, joto kali lilikausha mimea yote, mito ilikauka, misitu iliwaka moto na watu wengi walikufa.

Houyi alishawishi majua kumi yatokee moja moja kwa zamu, lakini yalikuwa hayasikii. Kwa kukasirika, Houyi alitungua majua tisa na kubakiza moja mbinguni.

Kutokana na wivu Houyi alisingiziwa na miungu mingine mbele ya mungu mkuu, basi mungu mkuu alimwadhibu Houyi abaki duniani pamoja na mkewe. Lakini mke wa Houyi alishindwa kuishi maisha magumu duniani.

Houyi alisikia kwamba kuna dawa ya ajabu kwenye mlima wa Kunlun, mtu akila dawa hiyo ataweza kuruka mbinguni. Houyi alisafiri mbali kwa shida, na mwishowe aliipata dawa hiyo. Lakini dawa hiyo inaweza kutumiwa na mtu mmoja tu, kutokana na kutotaka kuachana na mke wake Chang E, Houyi alificha dawa hiyo.

Katika tarehe 15 Agosti Chang E alitumia fursa ya mume wake kutokuwepo nyumbani alikula dawa hiyo na mara akapaa mbinguni hadi mwezini.

Houyi aliishi duniani kwa kuwinda, aliwapokea wanafunzi kadhaa kuwafundisha upigaji mishale. Kati ya wanafunzi hao alikuwako mmoja aliyeitwa Peng Meng, alipata maendeleo makubwa katika upigaji mishale. Mwanafunzi alifikiri kuwa kama Houyi akiwa hai basi yeye daima atakuwa wa pili katika upigaji mishale, basi alitumia fursa ya Houyi kulewa alimwua Houyi.

Chang E aliishi peke yake mwezini ila tu sungura mmoja mweupe na mti mmoja mkubwa, alimkumbuka mumewe hasa katika siku ya tarehe 15 mwezi Agosti.