Gun na Dayu Wadhibiti Maji
中国国际广播电台


      Nchini China “hadithi ya Dayu kudhibiti maji” ni maarufu kwa wote, lakini sio wengi wanaojua kuwa baba yake Gun naye pia ni shujaa wa kudhibiti maji. Leo katika kipindi hiki nitawajulisheni hadithi ya watu hao wawili, baba na mwana walivyodhibiti maji.

Katika siku za kale China ilikumbwa na mafuriko kwa muda wa miaka 22, ardhi ilikuwa bahari tupu, mimea yote ilizama ndani ya maji, watu hawakuwa na sehemu ya kukaa, hawakuwa na tegemeo lolote katika maisha, na idadi yao ikapungua haraka. Hali hiyo ilimfadhaisha sana mfalme Yao. siku moja aliwakusanya watemi wote kujadiliana na mwishowe alimwagiza Gun kudhibiti maji.

Baada ya kupewa jukumu hilo, Gun alitafakari sana, kwa bahati akakumbuka usemi mmoja wa wenyeji, kwamba “Wavamizi wakija wadhibitiwe na jemadari, na maji yakija yakingwe kwa udongo”. Akapata wazo kuwa kama kijiji kikizungushiwa boma si maji yatabaki nje? Lakini ardhi yote ilikuwa imejaa maji, angewezaje kupata udongo? Wakati huo kobe moja aliibuka akamwambia Gun: “Nyumbani kwa mungu kuna kitu kimoja kiitwacho ‘Xi Rang', ukikipata na kukitupa majini kitakua na kuwa boma na mlima.” Baada ya kusikia hayo Gun alifurahi mno, akamuaga kobe na kuanza safari yake.

Gun alitaabika sana katika safari yake ndefu, lakini mwishowe alifika nyumbani kwa mungu. Alimsihi mungu ampe kile kitu kiitwacho “Xi Rang” akitumie kudhibiti maji ili kuwaokoa wananchi. Lakini mungu alikataa. Kutokana na jinsi alivyowakumbuka wananchi walivyohatarishwa na maafa ya mafuriko ya maji, Gun alitumia fursa ya uzembe wa walinzi na kuiba kile “Xi Rang” na kurudi nacho nyumbani. Akakitupa “Xi Rang” majini, kweli kikakua haraka, maji yakipanda juu nacho kikakua zaidi, maji yakazuiliwa nje ya boma. Watu walifurahi huku wakirukaruka, wakaanza kulima mashamba.

Lakini baadaye mungu aligundua kwamba “Xi Rang” kimeibwa. Akawatuma askari wake mara moja kukirudisha. Maji yakajaa tena, boma likaporomoka, mashamba yakazama, na watu wengi wakafa maji. Mfalme Yao alikasirika sana, akasema, “Gun anajua tu kujenga boma kuzuia maji, na boma linapoporomoka maji yanakuwa mengi zaidi. Amejaribu kudhibiti maji kwa miaka 9 lakini hakufanikiwa chochote, anastahili kuuawa!” Gun akatiwa gerezani, na baada ya miaka mitatu aliuawa akiwa na hasira ya kuonewa.

Baada ya miaka 20, mfalme Yao alimrithisha Shun kiti cha enzi yake, mfalme Shun alimtuma mtoto wa kwanza wa Gun, Da Yu, kwenda kudhibiti maji, ambapo mungu alikubali kumpa Da Yu kitu chake “Xi Rang”. Mwanzoni Da Yu pia alidhibiti maji kama alivyofanya baba yake, lakini kila baada ya kujenga boma lake mara lilibomolewa na maji makubwa, baada ya majaribio ya mara nyingi akatambua kuwa, “Kuzuia tu maji hakutoshi, lazima yazuiliwe katika sehemu inapofaa na kutoka kwenye sehemu inayohitajika.”

Da Yu alipanda mgongoni kobe mkubwa akiwa na “Xi Rang” huku akielea huku na huko, ambapo alitumia “Xi Rang” kwenye sehemu iliyodidimia na sehemu ilipokaliwa na watu, pia alichimba mito kupeleka maji baharini. Inasemekana kuwa, Da Yu kwa kudura ya mungu alipasua na kukata kata milima ili maji yapite, hivyo yakapatikana magenge matatu ya San Menxia ya leo. Tokea hapo kwa zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, magenge matatu ya San Menxia yamekuwa yakivutia watalii kwa maji yake yanayokwenda kwa kasi kubwa.

Hadithi simulizi kuhusu Da Yu ni nyingi, watu wanasema, Da Yu alimwacha mkewe siku nne tu baada ya kumwoa kwenda kudhibiti maji, na katika muda wake wa miaka 13 wa kudhibiti maji alipita nje ya nyumbani kwake mara tatu lakini hakuingia. Kwa juhudi zake za kupambana na matatizo mengi, mwishowe alifanikiwa kudhibiti maji, wananchi wakaanza kuishi bila wasiwasi. Kama shukrani, wananchi walimwunga mkono awe mfalme, na mfalme Shun alimwachia kiti chake kwa hiari kutokana na mafanikio yake makubwa.

Katika jamii ya kale, uwezo wa binadamu ulikuwa dhaifu sana. Binadamu wanapopambana na maafa ya maumbile pia walitunga hadithi nyingi za ajabu ajabu kuonyesha matumaini yao. Gun na Da Yu ni mashujaa walioumbwa na watu katika mapambano dhidi ya maafa ya mafuriko, na ndani ya hadithi, shida walizopata mashujaa pia ni matatizo yanayowakabili wanapopambana na mafuriko. Mwishowe watu wametambua kuwa kudhibiti maji lazima watumie njia mbili kwa pamoja, yaani “kuzuia na kutoa”.