Hadithi ya Msichana Hou Ji na Mazao Yake
中国国际广播电台

Ustaarabu wa China ya kale ni wa kilimo, kwa hiyo, yapo masimulizi mengi yanayohusiana na shughuli za kilimo. Leo katika kipindi hiki nimewaletea “hadithi ya msichana Hou Ji na mazao yake”.

Baada ya binadamu kutokea duniani walikuwa wakiishi kwa kutegemea uwindaji, uvuvi na kukusanya matunda mwituni. Walikuwa mbioni wakati wote ili kupata riziki, hata hivyo walikuwa hawakosi kulala na njaa.

Alikuweko msichana mmoja alijulikanaye kama ni Jiang Yuan. Siku moja alicheza nje, alipokuwa akirudi nyumbani aligundua unyayo mmoja mkubwa kwenye kinamasi, alishangaa akaukanyaga. Mguu wake ulipogusa tu ule unyayo mara akasikia msisimko mwili mzima. Muda si muda baadaye akapata ujauzito.

Siku zilipita haraka, Jiang Yuan alijifungua mtoto wa kiume. Kwa kuwa mtoto huyo alikuwa hana baba, majirani walimwona kama kisirani, basi wakamnyakua kutoka kifuani kwa mama yake wakamtupa makondeni wakidhani kuwa angekufa kwa njaa. Lakini kwa bahati nzuri wanyama waliopita walimwokoa, baadhi ya wanyama jike walimnyonyesha maziwa. Baada ya kusikia habari hiyo majirani walitaka kumwacha misituni, lakini walipotaka kumtelekeza walitokea watema kuni, wakaacha nia yao. Mwishowe majirani kwa hasira waliazimia kumtupa kwenye barafu, lakini kabla majirani hawajafika mbali ndege wakubwa walishuka na kumhifadhi kwenye mabawa yao. Hapo ndipo majirani walipotambua kuwa mtoto huyo hakuwa wa kawaida, wakamrudisha kwa mama yake. Kutokana na mtoto huyo kutupwa mara kadhaa, mama yake alimpatia jina la “telekezo”.

Tokea utotoni mtoto huyu alikuwa na ari kubwa. Aliona watu kila siku wakihangaika huku na huko kujitafutia riziki bila kuweza kuishi katika sehemu maalumu, wazo lilimjia akilini: ingekuwa bora kupata sehemu ya kuzalisha chakula. Kwa kuchunguza chunguza, alikusanya mbegu za ngano, mpunga, kunde, mtama na kokwa za matunda mwituni na kupanda katika shamba lake alilofyeka, alimwagilia maji na kupalilia kila baada ya muda fulani. Baada ya mimea kuiva, mazao aliyovuna yalikuwa mazuri na matamu kuliko ya misituni. Ili kurahisisha kazi alitengeneza zana za kulimia kwa miti na mawe. Alipofikia utu uzima, alikuwa amepata uzoefu mkubwa katika kilimo.

Msichana Telekezo aliwaelimisha majirani uzoefu wake wote bila ya kubania, basi tokea hapo watu wakaacha maisha ya kuhama hama ya uwindaji, uvuvi na kujitafutia matunda mwituni. Kwa heshima watu walimpatia jina “Hou Ji” badala ya Telekezo, maana yake ni Malkia wa Mazao.

Baada ya kufariki dunia, Hou Ji alizikwa katika sehemu yenye mandhari nzuri karibu na ngazi ya kuendea peponi. Miungu walipanda na kushuka kwa ngazi hiyo, sehemu hiyo ardhi yake ilikuwa na rutuba nyingi, mimea ilistawi na ndege wengi waliruka na kuimba angani katika majira ya mavuno.