Kuongeza Miguu kwenye Picha ya Nyoka

中国国际广播电台

Katika zama za kale, alikuwepo tajiri mmoja katika Dola la Chu. Siku moja tajiri huyo alifanya tambiko kwa babu yake, kisha aliwashukuru wasaidizi wake kwa bilauri moja la pombe. Wasaidizi walishauriana na kusema, “Bilauri moja ya pombe haitoshi kwa wote na inazidi kwa mmoja. Basi tuchore nyoka ardhini, mtu atakayetangulia kumaliza kuchora atastahili kunywa pombe hiyo.”

Kati yao mmoja alimaliza mapema, akachukua bilauri akitaka kunywa kwa kujipongeza, alishika bilauri kwa mkono wa kushoto na kwa mkono wa kulia aliendelea kuchora akisema, “Mnaona, hata nina nafasi ya kuongeza miguu kwenye picha yangu ya nyoka!”

Lakini kabla hajamaliza kuchora miguu, mwingine alipokonya bilauri na kusema, “Nyoka hana miguu!” Kisha akanywa pombe yote. Mtu aliyetangulia kumaliza picha ya nyoka alikosa bilauri yake ya pombe.

Hekaya hiyo inawaambia watu kwamba kila jambo lina kigezo chake, na asileweshwe na ushindi na kusababisha kushindwa.