Kuficha Ugonjwa kwa Kuogopa Matibabu
中国国际广播电台

Katika China ya kale ya Enzi za Madola ya Kivita alikuwako daktari mmoja maarufu katika Dola la Qi, jina lake Qin Yueren. Lakini badala ya kumwita jina lake hili halisi watu humwita Bian Que. Bian Que alikuwa daktari wa ajabu katika hadithi za mapokeo ya kale, magonjwa yoyote aliweza kuponyesha.

Kutoka uzoefu wa muda mrefu, daktari Bian Que alikuwa ameratibisha njia zake za kugundua ugonjwa, yaani kuangalia, kunusia, kuuliza na kupima vipigo vya mshipa wa damu. Hasa uhudari wake wa kuangalia, yeye kwa kuangalia ngozi, sura na vitendo angeweza kujua fulani ana ugonjwa gani na kwenye sehemu gani.

Siku moja alikuja mji mkuu wa Dola la Qi, Mfalme Huan alimkaribisha katika kasri yake. Bian Que alipomsalimu aligundua mfalme amepata ugonjwa. Basi akamwambia kinaganaga, “Umekuwa mgonjwa, sasa ugonjwa unaanza tu kwenye ngozi yako, lakini usipotibiwa ugonjwa utazidi.”

Mfalme Huan alifikiri: Ni wazi mimi mzima kabisa, ugonjwa unatokea wape? Kumbe huyu daktari uhodari wake ni jina tu. Akamwambia, “Sina ugonjwa wowote.” Baada ya Bian Que kuondoka, mfalme kwa dhihaka aliwaambia mawaziri wake walio pembeni, “Madaktari huwa na tabia ya kufafuta dosari ili kuonyesha uhodari wao. Anang'ang'ania kukuambia u mgonjwa, hali u mzima kabisa!”

Bian Que alikuwa na wasiwasi juu ya ugonjwa wa mfalme, baada ya siku tano, alienda tena kumwangalia, alisema, “Ugonjwa wako ushaingia ndani ya misuli yako, usipotibiwa ugonjwa utazidi zaidi!” Mfalme akamjibu kibaridi, “Unachosema sina.” Kisha akamwondoa kwa kisingizio.

Siku tano zingine zikapita, daktari huyo mwenye roho teketeke kwa mara ya tatu alimwendea Mfalme Huan. Aliona kweli ugonjwa ukawa umezidi sana. Bila kujali alivyoumbulika alimhadharisha mfalme, “Ugonjwa wako umeenea mpaka tumboni sasa, ukichelewa zaidi utajingiza hatarini!” Mfalme Huan alinyamaza tu kwa hasira. Bian Que alikuwa hana budi ila kuondoka.

Siku tano nyingine zaidi zikapita, daktari hakuweza kutuliza moyo wake juu ya ugonjwa wa Mfalme Huan, akamwendea tena. Lakini alipomwona tu mfalme mara akageuka nyuma bila neno lolote. Awali mfalme alidhani pengine huyo daktari angepayuka tena, kumbe aliondoka kimya, akaona ajabu, akamrudisha na kumwuliza, “Mara hii mbona hukuniachia hata neno moja?”

Daktari alimjibu, “Ugonjwa ukiwa kwenye ngozi unaweza kuponyeshwa kwa maji vuguvugu, ukiwa kwenye misuli unaweza kuponyeshwa kwa akyupankcha, ukiwa kwenye tumbo dawa za mitishamba zaweza kuponyesha. Lakini ugonjwa ukienea mpaka ndani ya uboho, basi uwezo wangu umekwisha!”

Siku tano zikapita tena, kweli Mfalme Huan alianza kuugua mwili mzima, hapo akaamini aliyoambiwa na daktari, kwa haraka akatuma mtu kumwalika, lakini wakati huo Bian Que alikuwa ameondoka Dola la Qi. Siku chache baadaye mfalme akatupa mkono.

Watu wa baadaye wamefupisha kisa hiki kuwa msemo wa “Kuficha ugonjwa kwa kuogopa matibabu”. Maana yake ya ndani inaeleza kwamba fulani ana makosa lakini hakubali anapoambiwa, basi matokeo yake yatakuwa mabaya zaidi.