Bweha Aazima Ukali wa Chui
中国国际广播电台

Kipindi kati ya karne ya tano mpaka ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristu, kilikuwa ni "Enzi ya Madola ya Kivita" katika historia ya China, kwa sababu wakati huo yalikuwako madola kadha, na mapambano yalikuwa hayaishi baina yao. Lakini katika nyakati hizo dhana za aina mbalimbali pia zilikuwa zikiibuka zikawa chanzo cha aina nyingi za utamaduni wa China zikiwa ni pamoja na nahau nyingi. Katika kipindi hiki, nitawasimulieni hadithi ya nahau moja: "Bweha Aazima Ukali wa Chui".

Dola la Chu lilikuwa nchi yenye nguvu zaidi kuliko mengine katika kipindi cha mwisho cha Enzi ya Madola ya Kivita. Alikuwako jemadari aitwaye Zhao Xixu aliyekuwa hodari sana. chini ya mfalme wa dola hilo Chu Xuan wang. Katika maingiliano na madola mengine dhaifu, mfalme huyo aligundua kwamba watu walikuwa wanamwongopa jemadari wake kuliko yeye mwenyewe. Aliona ajabu, basi akawauliza mawaziri wake sababu yenyewe.

Waziri mmoja aliyeitwa Jiang Yi alimsimulia hadithi ifuatayo.

Katika mlima mmoja aliishi chui mmoja kutokana na kubanwa na njaa alihangaika kutafuta mawindo yake huku na huko. Alipopita kwenye msitu mmoja mnene alimkuta bweha mmoja akitembeatembea mbele yake. Chui alifurahia bahati yake, akamrukia na kumkamata papo hapo.

Lakini alipofungua kinywa tayari kumng'ata ghafla bweha alinena, "Thubutu! Usidhani wewe ni mfalme wa wanyama, jua kwamba mimi nimeteuliwa na mungu kuwa mfalme wa wanyama wote. Yeyote atakayenidhuru ataadhibiwa vibaya sana.”

Kusikia hayo, chui alishtuka, ujeuri wake ukamtoka karibu nusu. Hata hivyo, alijawa na wahka, akafikiri: Kwa kuwa mimi ni mfalme wa wanyama, yeyote aliyeniona huniogopa. Sasa, bweha anadai yeye ndiye mfalme mteule wa kututawala. Ni kweli hayo lakini?

Wakati huo, bweha aliona chui anasitasita asithubutu kumwua, akabaini kwamba amemwamini kiasi, mara akabenua kifua akimwonyesha kidole puani na kusema, "Kwani huniamini nisemayo? Basi nifuate uone jinsi wanyama watakavyonikimbia kwa hofu." Chui aliona wazo hili si baya, akamfuata.

Bweha alitangulia mbele kwa maringo, na chui akimfuata nyuma kwa hadhari. Kabla hawajafika mbali, waliona msitu mbele yao, pale wanyama wadogo wadogo walikuwa wakitafuta riziki yao. Walipoona chui nyuma ya bweha wote wakakimbia ili kuokoa roho zao.

Bweha aligeuza kichwa kuangalia nyuma, akamtupia macho kwa kiburi. Kuona hali hiyo chui pia aliingiwa na hofu, hakujua kwamba waliyemwogopa si bweha bali ni yeye mwenyewe.

Baada ya kusikiliza hadithi hiyo mfalme Chu Xuanwang alitafakari, akatambua kwamba sababu hasa ya watu kumhofia jemadari Zhao Xixue ni yeye mwenyewe. Lakini huyo jemadari anamiliki madaraka ya kijeshi, hii itakuwa hatari kwake kama si leo basi ni kesho. Kufikiri hivyo akadhoofisha madaraka yake.

Kwa miaka mingi nahau ya "Bweha Aazima Ukali wa Chui" ikawa moja katika lugha ya Kichina ikimaanisha wale walioegemea madaraka ya wakubwa kufanya ujeuri.