Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan
中国国际广播电台


      Hadithi ya "Mvuvi na Shetani" kutoka "Elfu lela u lela" inajulikana kote duniani. Lakini pia iko hadithi nyingine ambayo inafanana na hadithi hii inasimuliwa sana duniani. Hii ni hadithi iitwayo "Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan".

Hadithi hiyo inatokana na kitabu kilichotungwa na Ma Zhongxi katika Enzi ya Ming, karne ya 13. Hadithi yenyewe ni kama ifuatayo:

Hapo kale alikuwako msomi mmoja Dong Guo, huyu bwana macho yake yalikuwa hayabanduki kwenye vitabu vyake kila siku na kila wakati. Hivyo akawa mbukuzi na elimu yake ilikuwa ya kitabuni tu. Siku moja akiwa na mfuko wake wa vitabu mgongoni alitoka na punda wake akienda mahali paitwapo Zhong Shan kutafuta nafasi ya udiwani.

Ghafla mbwa-mwitu mmoja aliyejeruhiwa alitokea mbele yake na kumsihi, "Ewe bwana, nafukuzwa na mwindaji, nilipigwa mshale, karibu nife. Naomba unifiche ndani ya mfuko wako. Nakuahidi nitakulipa kwa wema wako."

Bwana Dong Guo alijua mbwa-mwitu ni madhara kwa binadamu, lakini kuona alivyokuwa maskini, alimhurumia, alisita kidogo, lakini akamwambia, "Nikifanya kama usemavyo nitamkosea mwindaji, lakini basi nitakuokoa." Kisha akamwambia mbwa-mwitu ajikunyate, akamfunga miguu yake na kumwingiza kwenye mfuko.

Punde si punde mwindaji alikuja akaona mbwa-mwitu katoweka. Alimwuliza Bwana Dong Guo: "Je umemwona mbwa-mwitu kupita hapa? Amekimbilia wapi?"

Bwana Dong Guo alimjibu, "Hataa, sikumwona. Hapa njia panda ni nyingi, pengine amechukua njia nyingine." Mwindaji akamwamini, akafuata njia nyingine kuendelea kusaka.

Kusikia vishindo vya mwindaji na farasi wake vimekwenda mbali, mbwa-mwitu alimsihi Bwana Dongo Guo mfukoni "Naomba uniachie huru nikimbize roho haraka!"

Mwenye rehema Dong Guo alidanganywa na maneno ya mbwa mwitu, akamtoa mfukoni. Lakini ghafla, huyo mbwa-mwitu akamgeukia na kusema kwa kelele, "Sasa nabanwa na njaa, ilivyokuwa umenifanyia wema, basi unifanyie zaidi, nikumalize." Papo hapo akamrukia. Bwana Dong Guo alikukurushana naye, huku akiguta, "Usiye na fadhila we!"

Wakati huo, mkulima mmoja alipita hapo alikuwa na jembe mkononi. Bwana Dong Guo alimsimamisha na kumweleza kisa chenyewe, lakini mbwa-mwitu alikana kwamba aliokolewa naye. Baada ya kutafakari, mkulima akasema: "Hata mimi siamini wewe bwana ungeweza kumficha ndani ya mfuko wako mdogo kama huu, au umfiche tena nione." Mbwa-mwitu kakubali, akalala chini akajikunyata mviringo akimwachia Dong Guo amfunge miguu yake kwa kamba na kumwingiza mfukoni. Kwa haraka mkulima akafunga kabisa mfuko huku akimwambia Bwana Dong Guo, "Unadhani mnyama kama huyu angeweza kubadili tabia yake asimdhuru binadamu? Asilan! Ni ujinga kuwa na huruma kwa mbwa-mwitu!" Kisha akainua jembe lake akamwua kabisa mbwa-mwitu. Bwana Dong Guo akaerevuka na kumshukuru sana kwa kumwokoa.

"Bwana Dong Guo na Mbwa-mwitu wa Zhong Shan" imekuwa hadithi ya mafunzo: "Bwana Dong Guo" anawakilisha watu wababaishaji wa jema na baya na kutumia ovyo huruma; "mbwa-mwitu wa Zhong Shan" anawakilisha watu wasio na shukrani.