Hadithi kuhusu Ziwa la Xihu
中国国际广播电台

Ziwa la Xihu liko katika mji wa Hangzhou, mashariki mwa China. Katika karne ya 14, mtalii wa Itali Makopolo alipotembelea huko alisifu, “Mtu akiwa huko anajiona kama yuko peponi.”

Ziwa la Xihu linazungukwa na mlima kwa pande tatu, mandhari yake inavutia sana. Washairi mashuhuri wa kale karibu wote waliwahi kufika huko na kuandika mashairi kusifu mandhari ya huko.

Ziwa la Xihu likitajwa watu hukumbuka mandhari katika sehemu kumi toka jua linapochomoza mpaka linapozama.

Kuna masimulizi mengi kuhusu Ziwa la Xihu. Moja kati ya masimulizi hayo ni “Daraja Lililokatika”, au kwa jina jingine ni “Hadithi ya Joka Jeupe”.

Inasemekana kwamba kulikuwa na majoka mawili yenye miaka elfu moja, ambyo yalijigeuza kuwa wasichana wawili na kuja kwenye Ziwa la Xihu kujiburudisha. Walipofika kwenye daraja lililokatika msichana aliyekuwa joka jeupye alimkuta msomi mmoja, akampenda moyoni, wakati huo mvua kubwa ilikuwa inanyesha, msomi alijikinga mvua kwa mwavuli kwenye kando ya mashua.

Msomi huyo alipowaona wasichana hao walikuwa wamelowa mvua, aliwaazima mwavuli na yeye mwenye aliacha mvua imnyeshee. Yeye alimpenda zaidi msichana mwenye asili ya joka jeupe. Kwa msaada wa msichana mwenye asili ya joka jeusi, wao walioana. Baada ya ndoa msichana Joka jeupe alifungua duka la dawa na alipendwa sana na wenyeji.

Sufii aitwaye Fa Hai alifahamu wasichana hao walikuwa majoka, kisirisiri alimwambia msomi huyo. Sufii alimwambia, amshawishi mkewe anywe pombe katika siku fulani, akiwa joka atajirudisha asili yake. Baada ya kunywa pombe, mkewe kweli alijirudisha kuwa joka, msomi alipoona jinsi mke alivyo alikufa kwa hofu. Ili kumwokoa mumewe joka jeupe lilisafiri kwenda mbali kwa shida na kufika kwenye mlima mmoja ambako inasemekana kwamba kuna majani ya dawa ya kuweza kumwokoa mumewe. Baada ya kutumia dawa hiyo, mumewe alifufuka.

Katika siku asipokuwepo joka jeupe, Fa Hai alimdanganya msomi kwenda kwenye hekalu na kumzuia huko asiweze kurudi nyumbani. Wasichana hao wawili walikwenda kwenye hekalu kumrudisha msomi, katika purukushani mke wa msomi alipigwa, kwa sababu alikuwa karibu kuzaa, alikimbia kwa kulindwa na mwenzake joka jeusi.

Walipofika kwenye daraja lililokatika, walimkuta msomi. Hao mume na mke walikumbatiana na kulia sana. Wakati huo Fa Hai alikuja na kumkamata joka jeupe na kumzika chini ya pagoda ya Leifeng.

Baada ya miaka mingi kupita, joka jeusi alijipatia uhodari wa kupigana, alirudi kwenye ziwa la Xihu, alimshinda Fa Hai na kukausha maji ya ziwa la Xihu, aliangusha pagoda ya Leifeng na kumwokoa joka jeupe.

Hadithi ya kuachana na kukutana kwa msomi na mkewe inasimuliwa miaka hadi miaka, na kila watu wanapofika kwenye ziwa la Xihu hukumbuka hadithi hiyo.