Hekalu la Yonghegong
中国国际广播电台

Mjini Beijing kuna jengo lenye mitindo ya makabila ya Wahan, Wamen, Wamongolia na Watibet, hilo ni hekalu la Yonghegong.

  Yonghegong ni hekalu la dini ya Buddha la madhehebu ya Tibet, eneo lake ni mita za mraba elfu 60, kuna vyumba zaidi ya elfu moja. Hekalu hilo lilijengwa na mfalme wa Enzi ya Qing, Kangxi, mwaka 1694 kwa ajili ya mtoto wake wa nne Yinzhenbeile, lakini mwaka 1723 mtoto huyo alirithi kiti cha ufalme na alihamia kasri la kifalme la Beijing, aliliacha hekalu hilo kwa dini ya Buddha ya madhehebu ya Tibet.

Madhehebu ya Tibet ya Dini ya Buddha yalianzishwa na Zhakba (1375-1419).

Vitu vya kale ndani ya hekalu hilo ni vingi. Kati ya vitu hivyo kuna “maajabu matatu”.

Ajabu la kwanza ni mlima wenye sanamu mia tano. Mlima huo una kimo cha mita 4 na urefu wa mita 3. Mlima huo ulichongwa kwa mbao. Kwenye mlima huo umechongwa mapango, vibanda, pagoda, miti, michirizi, ngazi na sanamu. Lakini bahati mbaya sanamu zilizokuwa mia tano hapo awali sasa zimebaki 449 baada ya miaka yenye vurugu za vita katika historia.

Ajabu la pili ni sanamu ya Buddha ndani ya ukumbi mkuu wa hekalu hilo. Kimo cha sanamu hiyo ni mita 26, kati ya mita hizo, mita nane ziko chini ya ardhi.

Sanamu hiyo juu ya ardhi ina urefu wa mita 18, kipenyo chake ni mita 8, uzito ni tani 100, ni sanamu kubwa kabisa duniani iliyochongwa kwa gogo zima. Mwaka 1979 sanamu ilipokarabatiwa, mafundi waligundua kwamba sehemu ya chini bado haijaoza.

Ajabu la tatu ni sanamu ya shaba, nyuma ya sanamu hiyo ni sahani kubwa ya shaba nyekundu yenye michongo ya miale ya jua, chini ya mwangaza, mishale inang'ara nyuma ya kichwa cha sanamu hiyo.

Kwenye nguzo mbili zilizo kando ya sanamu hiyo yalichongwa majoka 99 yaliyoonekana kama ya kweli.

Ndani ya ukumbi huo kuna pagoda tano zilizopakwa rangi ya dhahabu na jiwe kubwa lililochongwa kwa maandishi ya makabila manne ya Wahan, Waman, Wamongolia na Watibet. Tokea mwaka 1981 China ilipoanza kufungua mlango kiuchumi, kila mwaka watalii kiasi cha milioni wanatembelea hekalu hilo.