Pagoda ya Mbao Mkoani Shanxi
中国国际广播电台


      Nchini China kuna pagoda nyingi za dini ya Buddha. Dini ya Buddha nchini China ilianzia India, lakini pagoda ya dini ya Buddha imechanganya mtindo wa Kichina.

Pagoda ya mbao mkoani Shanxi ilianza kujengwa mwaka 1056 na kumalizika baada ya miaka 140. pagoda hiyo ilijengwa juu ya jukwaa lenye kimo cha mita 4, urefu wa pagoda hiyo ni mita 70 na shina lake lina kipenyo cha mita 30. Pagoda hiyo ilitumia mbao mita za ujazo 3000, uzito wake ni kiasi cha tani 3000.

Umbo la pagoda hiyo ni la pembe nane, lina matabaka 9 na nguzo 28 kwa nje na nguzo 8 kwa ndani.

Kwenye upenu wa kila tabaka kuna kengele, upepo unapovuma kengele hizo zinalia.

Tokea pagoda hiyo ijengwe hadi sasa, katika muda wa miaka zaidi ya 900, iliwahi kukumbwa na matetemeko mengi ya ardhi. Kutokana na rekodi ya historia, miaka 300 baada ya pagoda hiyo kumalizika kujengwa, lilitokea tetemeko kubwa la ardhi, na liliendelea kwa siku 7, lakini pagoda hiyo ilikuwa nzima.

Kabla ya ukombozi wa China, mabwana vita waliendelea kupambana, pagoda hiyo iliwahi kupigwa mabomu ya mzinga zaidi ya 200, lakini pagoda hiyo haikudhurika.

Uimara wa pagoda hiyo unatokana na usanifu wake wa kisayansi, fremu iliposanifiwa ilizingatia matetemeko ya ardhi, na sababu nyingine ni kuwa pagoda hiyo ilijengwa kwa mbao tupu ambazo zina tabia ya kunyumbulika.

Pagoda hiyo haikuwahi kupigwa na radi, kwa sababu ina waya nene iliyochomekwa ndani ya ardhi kwa kina, na pembezoni mwa pagoda hiyo pia kuna miyororo 8 ya chuma iliyofukiwa ndani ya ardhi.

Pagoda hiyo imeonesha wazi ufundi mkubwa wa mafundi wa China ya kale, na elimu kubwa ya uwiano na kinga dhidi ya radi.