Hadithi kuhusu jiwe la kaburi lisilo na maandishi
中国国际广播电台


    Mkoani Shanxi, magharibi mwa China, lipo kaburi moja lenye miaka zaidi ya elfu mbili sasa. Katika historia ndefu ya jamii ya kimwinyi ya China kaburi hilo ni la pekee na la ajabu kwa sababu ndani yake wamezikwa wafalme wawili, mfalme wa Enzi ya Tang aliyejulikana kama Li Zhi, na mfalme wa kike wa Enzi ya Zhou aliyejulikana kama Wu Zetian. Wafalme hao wawili licha ya kuwa wawakilishi wa enzi mbili lakini pia walikuwa mume na mke. Wu Zetian alikuwa mfalme pekee wa kike katika historia ya China, ambapo maisha yake yalikuwa na maajabu mengi. Baada ya kifo chake, mbele ya kaburi lake lilisimamishwa jiwe moja lakini halikuandikwa hata neno moja juu yake. Hivi leo maombi yamewasilishwa ya kuingiza kaburi hilo katika orodha ya kumbukumbu za utamaduni duniani. Ifuatayo ni hadithi juu ya jiwe hilo la kaburi.

Wu Zetian alizaliwa mwaka 624. Alipokuwa na umri wa miaka 14 alichaguliwa kuwa mjakazi wa mfalme wa pili wa Enzi ya Tang, yaani Tang Taizong. Wu Zetian alikuwa na tabia ya ukali na kufanya maamuzi bila kusita. Mathalan, mfalme Tang Taizong alikuwa na farasi mmoja mkali, hapana mtu yeyote aliyeweza kumfundisha, lakini Wu Zetian alimwambia mfalme wake, “Niachie mimi, lakini nataka mjeledi wa chuma na jambia. Kwanza nitajaribu kumfundisha kwa mjeledi, nikishindwa nitampiga kichwani, na nikishindwa tena nitamkata koo lake kwa jambia.” Ah, kusikia hayo mfalme Tang Taizong alishituka, akashangaa kuwa katika jamii ya kimwinyi yenye miiko mingi kwa wanawake hawapaswi kusema maneno kama hayo. Lakini mwana mfalme Li Zhe alimpenda sana mwanamke huyo aliyemzidi kwa miaka minne.

Baada ya mfalme Tang Taizong kufariki dunia, Wu Zetian akawa mtawa kufuatana na taratibu za kimwinyi, na mtoto wa mfalme Li Zhi akarithi kiti cha ufalme kwa jina la kifalme la Tang Gaozong. Li Zhi hakumsahau Wu Zetian hata siku moja, kwa hiyo muda si mrefu baadaye akamrudisha ndani ya kasri na kumfanya kuwa kijakazi wa kwanza. Lakini Wu Zetian alikuwa haridhiki na hali yake, akitamani sana kuwa mke halisi wa mfalme, basi akatega mtego wa kinyama. Mama Tang Gaozong alikuwa mgumba, lakini aliwapenda sana watoto. Siku moja alikwenda kumwangalia mtoto wa kike wa Wu Zetian aliyezaliwa siku chache zilizopita. Baada ya mke wa mfalme kuondoka tu chumbani mara Wu Zetian akamwua binti yake kwa kumkaba shingoni, kisha akamfunika kwa mfarishi kama kawaida. Baada ya dakika chache, mfalme Tang Gaozong aliingia ndani kumtazama mtoto wake, alipofunua mfarishi akagundua kwamba mtoto amekwishakata roho, alishangaa sana. Wakati huo Wu Zetian alikuwa akilia na kuzirai. Mfalme aliwadadisi vijakazi kutaka kujua mtu aliyewahi kuingia chumbani. Wote walimwambia hakuna yeyote ila mkewe. Mfalme alighadhibika vibaya, aliamini kwamba muuaji ni mkewe, na kuanzia hapo alimchukia sana, mwishowe alimwondoa na kumteua Wu Zetian kuwa mke wake.

Baada ya kupata hadhi ya kuwa mke wa mfalme, Wu Zetian alianza kushiriki katika shughuli za utawala bila kujali utaratibu wa kimwinyi ambao haukuruhusu wanawake kuingilia mambo ya serikali. Hatimaye mfalme alimwachia Wu Zetian madaraka yote, mawaziri wakawaita “watakatifu wawili”.

Baada ya mfalme Tang Gaozong kufariki, Wu Zetian alikuwa amejikusanyia madaraka yote, akajitawaza kuwa mfalme alipokuwa na umri wa miaka 67, akabadilisha enzi ya Tang kuwa Enzi ya Zhou. Alikuwa mtu mwenye umri mkubwa kuliko wengine alipochukua wadhifa wa kuwa mfalme na pia ni mfalme pekee wa kike katika historia ya China.

Baada ya Wu Zetian kuchukua madaraka, aliwalea maofisa wake kuwa wakatili kama yeye, kuwaua watu hovyo na kuondoa kabisa wale waliotofautiana naye kimawazo, aliwaua jamaa wote wenye nasaba ya wafalme wa Enzi ya Tang na hata mtoto wake wa kiume. Mawaziri Xu Jingye na Luo Binwang wa Enzi ya Tang walipania kurudisha utawala wa enzi ya zamani ya Tang, walifanya uasi katika mji wa Yang Zhou. Luo Binwang aliandika makala kumshutumu Wu Zetian na kutawanya kote nchini. Baada ya kuisoma Wu Zetian aliinamisha kichwa kwa tabasamu, akawauliza mawaziri, “Ni nani aliyeandika makala hii?” Mawaziri wakamwambia, “Luo Bingwang.” Akauliza zaidi, “Mtu hodari kama huyo mbona ameachwa vijijini?”, basi papo hapo akatuma askari laki tatu akawaua wote wawili baada ya kupigana vita nao.

Lakini tukimwangalia kutoka upande mwingine, Wu Zetian pia ana sifa nzuri, kwamba alitumia sera mwafaka kuendeleza kilimo, alieneza mfumo wa mtihani wa kifalme wa raia ambao ni mfumo wa kuchagua maofisa kutoka kwa raia, alithamini na kutumia watu hodari na alipandisha hadhi ya wanawake. Wu Zetian alikalia kiti cha mfalme kwa miaka 15, lakini hali ilivyo ni kuwa aliendesha utawala kwa nusu karne. Chini ya utawala wake, China ilikuwa imeimarika kwa nguvu, jamii ilikuwa ya utulivu, idadi ya watu iliongezeka, uchumi ulistawi, na mara kadhaa alisambaratisha mashambulizi ya maadui. Aliweza kuendeleza zaidi ustawi aliourithi kutoka Enzi ya Tang katika Enzi yake ya Zhou.

Wu Zetian aliishi miaka 82, mwili wake ulizikwa pamoja na mumewe mfalme Tang Gaozong, mbele ya kaburi lilisimamishwa jiwe moja lisilokuwa na maandishi yoyote. Hili ni jiwe kamili, lina urefu wa mita nane na upana wa mita mbili, na lina nakshi nzuri. Kutokana na jiwe hilo kutokuwa na maandishi yoyote limetokea kuwa maarufu sana. Kuna mawazo ya aina mbalimbali kuhusu jiwe hilo. Baadhi wanasema, jiwe hili liliachwa tupu kutokana na taabu ya Wu Zetian kujisifu, kwa sababu aliona sifa zake haziwezi kuelezwa kwa maneno; Baadhi wanasema kwamba yeye alipindua utaratibu wa wanaume kutawala, hivyo alijua kosa lake kubwa, kwa hiyo aliona hakuwa na sifa ya kujipatia jiwe lenye maandishi; Lakini baadhi wanasema tofauti kwamba wote waliozikwa ni wafalme, tena ni mume na mke, kwa hiyo upo utata wa cheo, ama ni mke wa mfalme Tang Gaozong wa Enzi ya Tang, au mfalme Wu Zetian wa Enzi ya Zhou. Kutoandika chochote juu yake ni mchepuo wa yote hayo kwa busara. Watu wengi zaidi wanaona kuwa kutoandika lolote ni ujanja wake, kwa kuwa yeye mwenye alijua watu wangekuwa na tathimini tofauti juu yake, na maneno yasingeweza kueleza jinsi maisha yake yalivyokuwa, kwa hiyo aliacha jiwe bila neno na kuwaachia watu wa baadaye wazungumze watakavyo.