Hadithi kuhusu Mlima Lushan
中国国际广播电台


   Mlima Lushan ulioko mkoani Jiangxi, kusini mwa China una mandhari ya kuvutia. Tokea enzi na dahari mlima huo unasimuliwa kwa hadithi nyingi.

Katika sehemu ya kaskazini mkoani Jiangxi, mlima huo unajulikana kwa sura zake nyingi za ajabu. Wasomi wengi waliwahi kutembelea mlima huo na waliacha mashairi mengi na picha nyingi. Mshairi mkubwa Li Bai aliyeishi katika karne ya nane Enzi ya Tang aliwahi kuandika shairi lake la kueleza maporomoko ya maji, “Chini ya jua moshi wa udi wapaa hewani kutoka mahekalu, kwa mbali maporomoko ya maji yaonekana kama yaanguka kutoka mbinguni.” Mwanafasihi mkubwa wa Enzi ya Song (960-1127) Su Shi alipotembelea mlima huo alieleza kuwa kutoka juu vilele vya mlima vinatofautiana kwa urefu, na huwezi kuona mlima huo Lu Shan ulivyo kwa sababu wewe upo ndani mlima huo.”

Inasemekana kwamba karne ya nne Enzi ya Zhou alikuwepo bwana mmoja aliyeitwa Kuang Su, alitawa katika mlima huo na kujaribu kupata uchawi. Mfalme wa Enzi ya Zhou aliposikia habari juu yake, alituma watu mara kadhaa kwenda mlimani kumwalika, lakini Kuang Su alikataa. Baadaye Kuan Su alitoweka, watu walidhani kuwa yeye amekuwa mungu, kwa hiyo watu waliupatia mlima huo kuwa jina jingine, Mlima Kuang.

Mwaka 381 sufii mmoja aitwaye Hui Yuan aliongoza wanafunzi wake kwenda huko na kujenga jumba la watawa linaloitwa Donglinsi, kwa hiyo mlima huo pia ni chanzo cha dini ya Buddha katika sehemu ya kusini ya China. Hui Yuan alikuwa huko kwa miaka 36, kutokana na kuwa aliwasimamia watawa kwa nidhamu kali aliheshimiwa sana.

Kuhusu jumba la Donglinsi na Hui Yuan mwenyewe pia kuna hadithi nyingi. Inasemekana kuwa jumba hilo lilipojengwa vifaa vya ujenzi viliishiwa, Hui Yuan alisumbua sana kila siku. Lakini ghafla siku moja radi ilipigwa mbinguni na mvua kubwa ilinyesha, watawa wote walizuiliwa nyumbani. Siku ya pili jua lilichomoza, na mbele yao lilitokea ziwa moja, na juu ya maji magogo mengi yalielea. Hui Yuan aliamini kuwa magogo hayo yaliletwa na mungu, kwa hiyo alitumia magogo hayo na kujenga ukumbi mmoja mkubwa.

Mbele ya jumba la Donglinsi kuna ziwa moja, na ndani ya ziwa hilo kuna mayungiyungi mengi, mandhari ilikuwa ya kuvutia sana. Inasemekana kuwamba ziwa hilo lilichimbwa na mtu mmoja aitwaye Xie Lingyuan. Huyo Xie Lingyuan alitaka kuwa mtawa lakini alikataliwa na Hui Yuan kwa kuona kuwa yeye sio mtu mtulivu. Hui Yuan alimwambia, afadhali achimbe ziwa moja na awe mtulivu kama maji ya ziwani, kisha atapokelewa kuwa mtawa. Kweli alichimba ziwa hilo na alipokelewa. Baada ya Hui Yuan kufariki, Xie Lingyuan alihuzunika sana, alimwandikia kumbukumbu kwenye jiwe mbele ya kaburi lake.

Licha ya utamaduni, mandhari ya kimaumbile ya Mlima Lushan pia inavutia sana, ni sehemu maarufu ya utalii.