Hadithi kuhusu Mlima Huangshan
中国国际广播电台


  Mlima Huangshan uko kusini mwa China, ni urithi wa kimaumbile duniani. Hapo awali mlima huo uliitwa Yishan, maana yake ni mlima mweusi. Lakini kwa nini baadaye umeitwa mlima Huangshan?

Katika masimulizi ya kale, Huangdi ni babu wa wazawa wa taifa la China, alikuwa mtawala kwa miaka zaidi ya mia moja, na alipendwa sana na watu wake. Baadaye kutokana kuzeeka sana, na yeye alikuwa hataki kuondoka duniani, basi baada ya kumwachia kiti chake cha ufalme kijana mmoja aitwaye Shao Hao alikwenda kutafuta njia ya kurefusha maisha yake.

Dini ya Dao ni dini pekee inayopatikana nchini China. Katika historia ya Dini ya Dao waumini walikuwa na mila ya kutengeneza dawa ya kurefusha maisha. Huandi alifuatana na wengine wawili kwenda kutafuta mahali panafaa kutengeneza dawa hiyo.

Walisafiri sana kila mahali nchini China na mwishowe walifika Mlima Yishan. Waliona mlima ulikuwa mrefu sana na hata ulichomeka mbinguni, na mawingu mwepesi ulikuwa kama shashi kila wakati, mabonde yalikuwa ya kina sana, waliona huko panafaa kutengeneza dawa ya kurefusha maisha.

Walikuwa kila siku wakichoma makaa na kutafuta mimea ya dawa mlimani, walichemsha mimea waliyochagua na kuchemsha siku hadi siku, mwaka hadi mwaka mpaka walipata dawa hiyo baada ya miaka 480. Huangdi alimeza donge moja, mara akaona mwili ukawa mwepesi, hata ndevu za mvi zikabadilika kuwa nyeusi, lakini makunyanzi yalikuwa bado yapo.

Wakati huo ghafla maji ya chemchemi ulitiririka kutoka mlimani, maji hayo yalikuwa mekundu na yenye harufu nzuri. Huangdi alioga kwa maji hayo kwa siku saba, ngozi yake ilikuwa laini na makunyanzi yalitoweka, alionekana kama kijana mbichi, Huangdi alikuwa hana wasiwasi wa kufariki. Tokea hapo Mlima Yishan ulipewa jina la Huangshan.

Mandhari inayovutia sana ni “kalamu yenye maua”. Ndani ya bonde kuna nguzo ndefu sana, sehemu yake ya chini ni ya mviringo kama kalamu, na sehemu ya juu ni nyembamba kama ncha ya kalamu, kwenye nguzo hiyo kuna miti misonobari ambayo ni kama maua, kwa hiyo watu husema “kalamu yenye maua”.

Inasemekana kwamba mshairi mkubwa wa kale Li Bai aliwahi kuota ndoto. Katika ndoto yake aliona mawingu yaliyoelea kama bahari na maua na majani yalistawi sana, ghafla kalamu kubwa ilichomeka kutoka baharini, na kalamu hiyo ilikuwa ndefu kama nguzo, aliwaza: itakuwa ni furaha kama angepata kalamu hiyo na bahari iwe wino.

Alipofikiri hivyo ghafla alisikia muziki na huku aliona miangaza yenye rangi mbalimbali ilitokea na kisha kwenye ncha ya kalamu yalichanua maua, alijaribu kufikia kalamu hiyo, lakini alipoikaribia alizinduka.

Baada ya kuzinduka, alikuwa akikumbuka ndoto yake, alitia nia ya kutafuta kalamu hiyo, mwishowe alifika Mlima Huangshan aliiona, alishituka na kusema, “Ala, kumbe kalamu niliyoota iko hapa.”

Inasemekana kwamba tokea alipoona kalamu hiyo, mashairi mazuri yalikuwa mengi chini ya kalamu yake.