“Mtenda Mabaya Hulipwa Mabaya”
中国国际广播电台


      Katika karne ya nane kabla ya kuzaliwa Kristo nchini China yalikuwako madola mengi yaliyokaa pamoja, mojawapo ilikuwa Dola ya Zheng. Malkia wa dola hiyo alijaliwa watoto wawili wa kiume: mkubwa aliitwa Wu Sheng, na mdogo Gong Shuduan. Kutokana na shida aliyoipata wakati wa uzazi wa kifunguamimba, malkia alimchukia Wu Shen na kumpendelea sana mwanawe mdogo, hata siku moja alimwomba mume wake mfalme akubali mwanawe huyo mdogo Gong Shuduan kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Mfalme alimkatalia kabisa. Baadaye mwanawe mkubwa Wu Sheng akatawazwa kuwa mfalme. Huyo ndiye mfalme “Zheng Zhuanggong” katika historia ya China.

Siku moja malkia alimtaka mfalme amgawie ndugu yake sehemu ya Jing, mfalme alikubali, na hivyo ndugu yake akahamia huko.

Kusikia habari hiyo mawaziri wakaenda kumshauri mfalme, “Sehemu ya Jing ni kubwa mno, huenda ikawa balaa kwa taifa. Kutokana na kanuni za mababu zetu, ukubwa wa mji mkubwa hauwezi kuzidi thuluthi moja ya mji mkuu, mji wa kiasi haufai kuzidi moja ya tano ya mji mkuu. Sasa eneo la Jing ni kubwa zaidi, hiyo hailingani na kanuni hata kidogo, baadaye utashindwa kuitawala.” Mfalme akajibu, “Njia nyingine sina. Hivyo ndivyo mama malkia anavyotaka, niwezaje kuepukana na janga hili?” Kusikia hayo, mawaziri wakapendekeza, “Ni heri kumpa sehemu nyingine ambayo ni rahisi kumdhibiti asiweze kukuza nguvu zake. Pindi nguvu zake zikiwa kubwa itakuwa ni shida kwetu kupamana nazo. Hebu fikiri kwamba hata magugu kichakani hayawezi kufyekwa yote sembuse ndugu yako anayedekezwa na mama yako!” Mfalme akajibu, “Mtenda mabaya hulipwa mabaya, mtaona wenyewe.”

Haukupita muda mrefu baada ya Gong Shuduan kuikalia shemu ya Jing akaanza kupanua zaidi na zaidi eneo lake la pembeni. Wakati huo mawaziri wakamwambia mfalme, “Dola moja haiwezi kumilikiwa na wawili kwa wakati mmoja, una ushauri gani sasa? Ikiwa utamwachia dola yetu, basi turuhusu tumhudumie yeye. La sivyo, tunaomba umwondoe kabisa huyu firauni ili isije ikawa ataungwa mkono na raia wa huko.” Mfalme akawaambia kwa utulivu, “Msiwe na wasiwasi, atajipeleka kwenye maangamizi.”

Kipindi kingine kikapita, Gong Shu alikuwa ameweka moja kwa moja sehemu ya Jing iliyopanuka chini ya himaya yake, utawala wa eneo lake ukawa maradufu kuliko hapo awali. Wakati huo mawaziri walishindwa kuvumilia, wakamwambia mfalme kinaga ubaga, “Ni wakati wa kumwondoa sasa, ama sivyo tutachelewa kabisa baada ya yeye kuungwa mkono na raia wa huko.” Lakini mfalme pia aliwaambia kwa utulivu, “Ilivyokuwa mambo yake yanakwenda kinyume cha uadilifu, atawezaje kuungwa mkono na raia wa huko? Uchoyo wake wa ardhi utamuua.”

Wakati huo Gong Shu alianza kushughulikia ujenzi wa kuta za mji, kuandikisha askari, akawa tayari kuushambulia mji mkuu. Alikula njama na mama yake ambayo atamwitikia kwa ndani kwamba atawafungulia askari wa mwanawe mdogo mlango wa mji mkuu. Habari hizo zilimfikia mfalme, akawaita mawaziri akawaambia kwa sauti thabiti, “Sasa wakati wetu umewadia.” Akaamrisha askari wake kushambulia sehemu ya Jing. Raia wa huko ambao toka awali walikuwa na nongwa mara walimsaliti Gong Shu walipowaona askari wa mfalme wakija. Gong Shu alikuwa hana mbele wala nyuma akatorokea dola nyingine.