“Unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa”
中国国际广播电台

Kichina kinapoeleza kuwa jambo fulani ni dogo, au ni sehemu ndogo kiasi cha kupuuzwa kulingana na kitu kizima huwa kinasemwa “unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa”, kana kwamba ni tone moja tu la maji katika bahari. Msemo huu unahusu mwanahistoria maarufu wa China ya kale Sima Qian.

SiMa Qian alizaliwa katika ukoo wa mrasimu mdogo mwaka 145 kabla ya Kristo. Baba yake alikuwa ofisa wa mambo ya historia. Kwa kuathiriwa na baba yake, Sima Qian alishikwa na hamu na historia tangu utotoni, alikuwa amesoma vitabu vingi, na kuanzia miaka yake 20 alianza kuzungukazunguka kila mahali kuchunguza watu walioandikwa katika vitabu vya historia, jiografia, na matukio, ambapo alijipatia elimu nyingi, hatimaye akawa mfuasi wa mfalme.

Wakati huo vita kati ya Dola ya Xiong Nu na Dola ya Han ilianza. Mfalme wa Dola ya Han, Liu Che akamchagua jemadari Li Ling kwenda mstari wa mbele kupigana na Xiong Nu. Jemadari huyu akiwa na askari elfu tano alipigana vita kishupavu. Mwanzoni, habari njema za matokeo ya vita zilikuwa zikimjia mfalme kwa mfululizo ambapo mawaziri wengi walimpongeza kwa uchaguzi wake wa hekima. Lakini baadaye hali ilikwenda kombo, jemadari huyo na askari wake walivamiwa pande zote; ingawa walipigana kufa na kupona kwa siku nane mfululizo lakini mwishowe wakauawa karibu wote. Naye jemadari akasalimu amri kwa Xiong Nu.

Kusikia hayo mfalme akakasirika mno, mawaziri waliomsifu uhodari wake wa uchaguzi hapo awali, wote wakaanza kumshutumu jemadari isipokuwa Sima Qian ambaye alikuwa mtulivu. Mfalme akamsaili mawazo yake. Sima Qian akamwambia moja kwa moja, “Li Ling alikuwa na askari elfu tano tu na alivamiwa na maadui zaidi ya elfu 80. Japokuwa hivyo alipigana nao mpaka akaishiwa na chakula, mishale na njia ya kurejea pia ilifungwa. Kwa hiyo Li Ling hakuwa amesalimu amri bali alikuwa akivizia nafasi mwafaka kujitolea kwa taifa. Naona mchango wake ni mkubwa kuliko kosa lake la kushindwa.”

Mfalme alipomsikia akimtetea akaghadhibika vibaya, akamtia gerezani papo hapo. Muda si muda baadaye fununu ikaja kwamba jemadari Li Ling amekuwa mwalimu wa askari wa Dola la Xiong Nu. Mfalme alihamaki mara moja, akamshikisha Sima Qian adabu kali ya kudhalilisha ya “kukatwa uume”. Kwa kuteswa vibaya hivyo Sima Qian alitamani hata kujiua, lakini baadaye wazo jingine lilimjia, akifikiri kwamba kifo cha mtu mdogo kama yeye hakingeleta huruma yoyote, badala yake pengine kingekuwa kicheko na burudani ya mazungumzo ya watu wanaokunywa chai. Kutokana na wazo hilo akapania kuvumilia aibu yake na kuamua kufunga kibwebwe kuandika kitabu kikubwa cha historia. Tokea hapo alitopea katika kazi hiyo na mwishowe akamaliza kitabu chake kikubwa kijulikanacho kama “Rekodi za Kihistoria”.

Sima Qian alidiriki kumwandikia barua rafiki yake mkubwa juu ya mawazo yake. Katika barua yake alifananisha kifo chake “ng'ombe tisa kupoteza unyoya mmoja tu”. Kutokana na maneno haya watu wa baadaye wakapata msemo wa “unyoya mmoja tu miongoni mwa manyoya ya ng'ombe tisa”.