Hadithi ya “Kutoboa Jani la Mti Kutoka Umbali wa Hatua Mia Moja”
中国国际广播电台

Nchini China katika Enzi ya Madola ya Kivita yaani kutoka mwaka 475 mpaka 221 kabla ya Kristo yalikuwako madola mengi madogo madogo kwa pamoja, na kila dola ilikuwa na watu wake mashuhuri ambao wanasimuliwa miongoni mwa watu hadi leo. Ifuatayo ni hadithi ya “Kutoboa Jani la Mti Kutoka Umbali wa Hatua Mia Moja”.

Bai Qi alikuwa hodari wa kupigana vita katika Dola ya Qin, kutokana na uhodari huo watu walimpachikia jina la “Jemadari Asiyeshindwa”. Mwaka fulani alitumwa na mfalme aongoze askari wake kuivamia Dola ya Wei. Vita dhidi ya Wei ikishinda, madola mengi yatadhurika mfululizo. Kwa hiyo vita hivyo viliwatia watu wasiwasi.

Alikuwako mshauri mmoja, aliyeitwa Su Li. Aliagizwa kwenda kumshawishi jemadari aache nia yake ya kuivamia Dola ya Wei. Kwa juhudi nyingi, mshauri huyo alifanikiwa kuonana na jemadari, akamsimulia hadithi ifuatayo:

Zamani za kale alikuwako mpiga mshale aliyeitwa Yang Youji. Alipata uhodari wa kupiga shabaha toka utotoni mwake, kiasi kwamba aliweza kutoboa jani la mti kutoka umbali wa hatua mia moja. Wakati huo huo alikuwako mtu mwingine ambaye pia alikuwa hodari wa kupiga mishale aliyeitwa Pan Hu. Siku moja watu hao wawili walikutana kwa bahati, na kila mmoja alikuwa na hamu ya kumshinda mwingine, hatimaye walitaka kupimana uhodari wao. Watu waliposikia habari hii, wengi walikuja kushuhudia mashindano yenyewe.

Dango liliwekwa umbali wa hatua mia moja na shabaha yenyewe ilikuwa mchoro wa moyo kwenye ubao mmoja. Pan Hu alifyatua mishale mitatu mfululizo, na kila mmoja ulilenga katikati ya moyo, ambapo watazamaji walimshangilia kwa mshangao. Baadaye ilikuwa zamu ya Yang Youji, aliangaza macho sehemu zote kisha akasema, “Hatua mia moja si mbali, shabaha ya mchoro wa moyo ni kubwa. Nashauri, tushindane kwa jani la mti kutoka umbali wa zaidi ya hatua mia moja.”

Akamwambia mtu mmoja apake jani moja rangi nyekundu, akafyatua mshale wake, jani lenye rangi nyekundu likatobolewa katikati.

Watazamaji wote walipigwa butwaa. Pang Hu alielewa fika kwamba uhodari kama huu hafui dafu, lakini pia hakuamini kuwa kweli Yang Youji angeweza kutoboa jani kila mara kwa umbali zaidi ya hatua mia? Kufikiri hivyo akaenda kwenye mti, akachagua majani matatu na kutia nambari kila moja kwa rangi. Alimwambia Yang Youji atoboe majani hayo matatu kwa mfululizo wa nambari.

Yang Youji alifika chini ya mti, akatambua kila jani kwa nambari yake, akarudi nyuma umbali wa hatua zaidi ya mia moja kutoka kwenye majani, akatia mshale kwenye upinde, akalifyatulia jani la kwanza, la pili na la tatu. Ah! mishale yote ilitoboa katikati ya majani kwa mfululizo wa nambari. Watazamaji wote walimshangilia kwa mayowe. Hapo ndipo Pang Hu aliridhika kabisa na uhodari wake.

Vifijo na vigelegele vilipozagaa uwanjani sauti ya mtu mmoja ilisikika kando ya Yang Youji, “Ehee, mtu hodari kama huyu ndiye anayestahili kufundishwa nami.”

Kusikia aliyosema, Yang Youji alikasirika, akamgeukia na kumwuliza, “Utanifundisha namna gani?”

Kwa utulivu mtu huyo alimjibu, “Mimi sitakufundisha namna ya kupiga mishale, bali nakuelewesha namna ya kuhakikisha sifa yako inakuwa ya kudumu. Je, uliwahi kufikiri kwamba endapo ukiishiwa nguvu au ukikosea shabaha walau kidogo, sifa yako itaporomoka? Mpiga shabaha hodari mwenye akili lazima alinde sifa yake.”

Mshauri Su Li baada ya kusimulia hadithi yake alimwambia Jemadari Bai Qi, “Wewe una sifa ya ‘jemadari asiyeshindwa', lakini haitakuwa rahisi kuishinda Dola ya Wei, ikiwa huwezi kuishinda mara moja, si utajiharibia sifa yako mwenyewe?” Jemadari Bai Qi aliposikia hayo aliyosema, kwa kisingizio cha kuumwa akaacha mashambulizi yake dhidi ya Dola ya Wei.