Hadithi ya “Mbawala Kuitwa Farasi”
中国国际广播电台

Hii ni hadithi ya Dola ya Qin ambayo ni dola ya kwanza kabisa ya jamii ya kimwinyi katika historia ya China.

Qin Shihuang, aliyekuwa mfalme wa kwanza wa Dola ya Qin, alikuwa na watoto wawili wa kiume, wa kwanza aliitwa Fu Su, ambaye alipelekwa kwenye sehemu ya mbali mpakani kusomeshwa baada ya kukomaa. Wa pili aliitwa Hu Hai, ambaye akiwa bado mdogo, mfalme alimpatia mwalimu myeka kumsomesha; mwalimu huyo aliitwa Zhao Gao.

Baada ya Dola ya Qin kufaulu kuunganisha China nzima ilistawi sana. Mfalme wa kwanza Qin Shihuang alikuwa na mazoea ya kutembeatembea kufanya ukaguzi huku na huko nchini akiwa na mawaziri wake huku akijisifu kwa mchango wake kwa kuchonga maneno yake kwenye mawe. Mwaka fulani aliugua akiwa safarini, na ugonjwa ukazidi mbaya, akaona siku zake zinahesabika, akamwagiza mwalimu myeka Zhao Gao kuandika wasia wa kumrithisha mwanawe wa kwanza Fu Su kiti cha ufalme. Siku chache baadaye mfalme wa kwanza Qin Shihuang akafariki dunia.

Lakini Zhao Gao alificha kabisa habari za kifo cha mfalme kwa maslahi yake mwenyewe. Aidha, kwa kugushi hati za mfalme aliandika wasia mwingine wa kumlazimisha Fu Su ajiue. Baadaye alirudi mji mkuu Xianyang na kumtawaza mfalme wa pili, Huhai ambaye alikuwa bado mdogo. Kwa kuwa mwalimu myeka wa mfalme wa pili, Zhao Gao alijiingiza kwenye kundi la kuamua mambo ya taifa bila ya matatizo.

Hata hivyo Zhao Gao hakuridhika, bali alizidi kumdhibiti mfalme mtoto, na alianza kutumia hila kuwaondoa wale wenye mawazo tofauti naye kisiasa. Alimwambia mfalme wa pili, “Utukufu wa mfalme unatokana mawaziri kutoruhusiwa kuonana naye kiholela. Wewe bado ni mdogo, kama maneno yako hayalingani na hadhi yako utachekwa na mawaziri, kwa hiyo ni busara kukaa ndani, na mambo yote niachie mimi, hivyo mawaziri hawataweza kukukanganya kwa makusudi.” Mfalme Hu Hai alikubali pendekezo lake, alijifungia ndani na ilikuwa nadra kuonana na mawaziri. Kwa kuwa alimdhibiti vilivyo mfalme wa pili, maofisa wote ndani ya kasri walimwogopa sana.

Lakini Zhao Gao aliendelea kuwa na wasiwasi hata mwishowe akaamua kutumia ujanja wa kupima utiifu wa kila mmoja ili awaondoe wale waliotofautiana naye kimawazo. Siku moja alimwagiza mtiifu wake mmoja alete mbawala na kusema mbele ya mfalme, “Nimekuletea farasi huyu kama zawadi.” Mfalme Hu Hai alidhani anamtania, akasema kwa tabasamu, “A,a, umekosea, mbona unamwita mbawala, farasi?” Lakini Zhao Gau alimjibu, “Kweli huyu ni farasi, ukiwa na wasiwasi, waulize mawaziri hawa.” Mfalme alipoona jinsi alivyomwambia kwa makini akashikwa na wahka. Akauliza mawaziri kadhaa. Baadhi yao walivungavunga bila ya kusema mbawala wala farasi, na baadhi yao walisema wazi kwamba ni farasi hasa. Alipoona hali hiyo mfalme akazidi kubabaika, akiwaza, jambo dogo na rahisi kama hili laleta mawazo tofauti miongoni mwa mawaziri, hii pengine inaashiria janga la taifa. Kisha mfalme alimwita ofisa wa sadaka, naye akamwambia mfalme kwamba hali hii imesababishwa na mfalme kutomwabudu sana mungu, akamshauri mfalme aondoke kwenye kasri akafunge saumu kwa muda katika sehemu tulivu. Mfalme akahamia bustani moja nje ya kasri, kwa kisingizio cha kufunga akajiburudisha kwa uwindaji huko.

Sasa, turudi kwa Zhao Gao. Baada ya mfalme wa pili kuondoka kwenye kasri Zhao Gao akawa mjeuri wa kufanya mambo atakavyo. Aliwafunga gerezani au kuwaua kisirisiri wale waliosema ukweli katika jaribio la “mbawala kuitwa farasi”.

Tokea hapo kasri ikawa kimya, hapakuwa na mpinzani wake hata moja. Hata hivyo hakuacha uchoyo wake, kwa sababu lengo lake ni kuwa mfalme halisi.

Muda si muda msukosuko ukatokea kote nchini, kwa kutumia fursa hii Zhao Gao alituma watu waliojifanya mahaini wavamie makazi ya mfalme na kumlazimisha ajiue. Baada ya yote hayo Zhao Gao alivumisha habari kwamba mfalme aliuwawa na mahaini, na dola haiwezi kukaa bila mfalme, kwa kuwa mfalme wa pili hana mtoto, yeye atakuwa mfalme. Mawaziri walikasirika mno, hakuna hata mmoja aliyemkubalia.

Baba mdogo wa mfalme wa pili alikuwa na nongwa toka zamani. Baada ya kupata habari kwamba kweli mpwa wake, mfalme wa pili, amekufa, alimwua Zhao Gao kwa njama, na yeye mwenyewe akawa mfalme wa tatu wa Dola ya Qin. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba baada ya siku 45 tu Dola ya Qin ikaangamizwa katika maasi ya wakulima. Ingawa Dola ya Qin iliangamizwa lakini hadithi ya msemo “Mbawala Kuitwa Farasi” ikawa simulizi, ikilenga wale watu wanaopindua ukweli na uwongo na kuwa na nia ya kufanya mambo mabaya.