“Utendaji wa Busara”
中国国际广播电台


       Kuanzia karne ya tano mpaka karne ya tatu kabla ya kuzaliwa Kristo ilikuwa enzi ya “Madola ya Kivita” katika historia ya China. Nyakati hizo yalikuwako madola mengi na yalikuwa mara kwa mara yakipigana vita kwa ajili ya kunyang'anyana ardhi. Vita vya muda mrefu viliwatokeza majemadari hodari na mahiri wengi wa mambo ya kijeshi, Sun Bin ni mmojawapo aliyejitokeza zaidi katika historia ya China. Haya, katika kipindi hiki nitawaelezeeni jinsi Sun Bin alivyotumia mbinu zake kuwashinda maadui.

Kabla ya kupata umaarufu, Sun Bin alikuwa na Pang Juan kusomea pamoja mbinu za kivita. Kisha baadaye Pang Juan akawa jemadari wa Dola ya Wei, lakini alitambua fika akilini kwamba umahiri wake haungefua dafu mbele ya Sun Bin. Kwa hiyo, aliwaza kwamba iwapo Sun Bin angekuja kwenye Dola ya Wei nafasi yake ya ujemadari hakika ingekuwa hatarini. Hivyo alimghilibu Sun Bin aje kwake. Baada ya Sun Bin kufika kwake, kwa hila alimkata miguu yake na akamtupa ndani ya zizi la nguruwe.

Kutokana na Sun Bin kujifanya mwendawazimu aliachiwa na mlinzi ambapo aliweza kuonana na mwakilishi wa Dola ya Qi kwa siri. Mwakilishi wa Qi alifurahia sana umahiri wake, akamsaidia kutorokea Dola ya Qi.

Mara baada ya Sun Bin kufika katika Dola ya Qi akapata heshima ya mfalme na kupewa cheo kikubwa.

Siku moja mfalme wa Dola ya Wei alimtuma Pang Juan na askari wake kushambulia Dola ya Han. Dola ya Han ikaiomba Dola ya Qi msaada. Mfalme wa Qi akawateua Tian Ji awe jemadari na Sun Bin awe mshauri wa kijeshi wakiambatana na askari kuisaidia Dola ya Han. Kwa ushauri wa Sun Bin askari wa Qi hawakuenda kwenye Dola ya Han iliyoomba msaada, badala yake walikwenda moja kwa moja katika Dola ya Wei kuushambulia mji mkuu wake Da Liang. Ili kuiokoa dola yake, Pang Juan aliacha mashambulizi yake dhidi ya Dola ya Han na kurejea haraka.

Sun Bin alipotambua kwamba Pang Juan amekwisharubuniwa, akamwambia jemadari wake, “Askari wa Dola ya Wei ni hodari zaidi, wanadharau askari wetu wakidhani wote wanaogopa vita, kwa hiyo watu hodari wa kupambana vita wanapaswa kutenda mambo kwa busara. Sasa basi, tujifanye kuogopa vita, turudi nyuma na kupunguza vishimo vya kuinjika sufuria kila siku, tuwaache maadui wakosee kuelewa ukweli ulivyo.” Kufuatana na mawazo yake, jemadari Tian Ji aliwaamrisha askari wake wachimbe vishimo laki moja vya kupikia kwa siku ya kwanza, elfu 50 kwa siku ya pili na elfu 30 kwa siku ya tatu.

Baada ya kugundua kwamba askari wa Qi wamerudi nyuma, Pang Juan akaamrisha mara moja askari wake wawafukuze moja kwa moja akitaka kuwaangamiza kwa pigo moja. Kila alipofika mahali askari wa Qi walipopiga mahema siku iliyotangulia Pang Juan huwaamrisha askari wake kuhesabu vishimo, na kugundua vishimo vikipungua siku hadi siku; hivyo alifurahi mno akidhani askari wa Qi wametoroka kwa kuhofia ukali wa askari wake, na sasa waliobaki ni wachache tu. Ili kumuua Sun Bin, Pang Juan alipiga mbio na askari wake wa farasi kwa kufuata alama alizoacha Sun Bin.

Wakati huo Sun Bin na askari wake walikuwa wamefika sehemu nzuri ya vita iitwayo Ma Ling, Sun Bin alionyesha kidole kuonyesha mti mmoja mkubwa na kuwaambia askari wake waondoe magome yote, na kuchonga maneno juu yake, “Pang Juan atakufa chini ya mti huu!”, kisha akawaamrisha tena askari hodari wa kupiga mishale wajifiche vichakani, na kuwaambia kwamba wapige mishale pale watakapoona moto.

Pang Juan alipofika Ma Ling usiku ulikuwa umeingia. Askari wake walikuwa hoi baada ya mwendo wa mchana kutwa, baada ya kushuka kwenye farasi mara wakajitafutia miti ya kuiegemea kwa ajili ya usingizi. Wakati huo mtu mmoja alipapasa ule mti wenye maneno, akapiga kelele. Pang Juan aliwaita askari walete mienge kumulika maneno, alipoyatambua tu yale maneno papo hapo mishale kemkem ikafyatuliwa huko. Askari wa Wei wakasambaratika na kutoroka ovyo. Hapo ndipo Pang Juan alipofahamu ameingia mtegoni. Lakini kwa kuzingirwa barabara na askari wa Qi, Pang Juan akawa hana njia, akajiua pale pale kwenye mti.

Hiki ndicho kisa maarufu “Mapambano ya Kiakili ya Sun Bin” katika historia ya China, msemo wa “Utendaji wa Busara” inatokana na kisa hicho.