Pu Songling na kitabu chake cha “Hadithi za Mashetani”  
中国国际广播电台


        Mwanzoni mwa karne ya 18, kitabu maarufu cha hadithi fupi fupi yaani “Hadithi za Mashetani” kiliibuka nchini China, Pu Songling kwa ustadi wake aliandika hadithi nyingi za mashetani na bweha.

Pu Songling alizaliwa mwaka 1640 na kufa mwaka 1715, alikuwa mwanafasihi katika Enzi ya Kifalme ya Qing. Alizaliwa katika ukoo wa wafanya biashara, lakini alifanya kazi ya ualimu. Katika maisha yake aliandika makala mengi na kitabu chake cha mkusanyiko wa hadithi fupi yaani “Hadithi za Mashetani” ndicho kilichompatia umaarufu.

Kitabu cha “Hadithi za Mashetani” kimekusanya hadithi 430, ambapo miongoni mwa hadithi hizo iliyo fupi kabisa ina maneno mia mbili au tatu hivi, na ile ndefu sana ina maelfu kadhaa ya maneno. Kitabu kizima kinaeleza hadithi za mashetani na bweha kikilaani pingu za maadili ya kimwinyi, ubovu wa mitihani ya kifalme ya kuchagua maofisa na kudai uhuru wa maisha ya binadamu. Katika kitabu hiki hadithi za kupendeza sana ni zile za mapenzi kati ya mashetani na bweha ambazo zilionyesha matumaini ya binadamu kuvunja pingu za maadili ya kimwinyi kati ya wanaume na wanawake.

Katika kitabu cha “Hadithi za Mashetani” bweha hujitokeza kama kisura. Miongoni mwa hadithi hizo, maarufu zaidi ni “Hadithi ya Xiao Cui”. Kwa kifupi hadithi hiyo inaeleza kama ifuatayo:

Alikuwako afisa mmoja aliyejulikana kama Wang Taichang, ambapo mtoto wake wa kiume Yuan Feng alikuwa punguani, na hapana hata msichana mmoja aliyekubali kuolewa naye, hali ambayo iliwasikitisha sana wazazi wake. Siku moja kwa ghafla walikuja nyumbani kwao mama mzee mmoja na binti yake. Mama mzee alisema kwamba kwa sababu ya umaskini anakubali kumwoza binti yake Xiao Cui kwa Yuan Feng. Kisha mama mzee huyo kwa kisingizio akaondoka nyumbani kwao na hakuonekana tena. Xiao Cui alikuwa msichana mwerevu, kila siku alicheza cheza na Yuan Feng bila kumchukia kutokana na utaahira wake. Wazazi wa Yuan Feng walimpenda sana mkamwana wao.

Alikuwako afisa mwingine, aliyejulikana kama Wang Jijian, ambapo alitaka kumtia hatiani Wang Taichang kwa kumsingizia, lakini Xiao Cui aligundua hila hiyo mapema. Alijipamba kama afisa mkubwa na kwa vishindo alimtembelea Wang Taichang, hivyo Wang Jijian aliona kwamba kumbe Wang Taichang ana tegemeo la afisa mkubwa, na ndipo akaacha hila yake ya kumsingizia. Familia ya Wang Taichang ikaepuka janga hilo.

Siku moja Xiao Cui alioga, kwa makusudi alimtosa mumewe Yuan Feng ndani ya maji ya moto. Wakwe zake walikasirika sana, lakini Xiao Cui hakutilia maanani akisema, Yuan Feng alikuwa punguani, afadhali afe kuliko kuishi. Maneno hayo yaliwakasirisha zaidi wakwe zake kiasi cha kutaka kumfukuza nyumbani, lakini wakati huo mtoto wao Yuan Feng alipona na kuwa mtu wa kawaida kabisa.

Baada ya miaka miwili kupita, mzee Wang Taichang alitaka kumhonga mtu fulani kwa jagi moja la thamani lakini kwa bahati mbaya Xiao Cui alilivunja, wazazi wakamshutumu na kumtukana Xiao Cui bila kujali wema aliowatendea. Kutokana na hilo Xiao Cui alijiua kwa kujitumbukiza kisimani.

Hadithi hiyo iliandikwa kwa vituko vingi vya kuwavutia wasomaji, ambapo mwandishi alimsawiri kwa ustadi msichana mmoja mwenye akili, roho nzuri na wa kupendeza. Mwishoni mwa hadithi hiyo mwandishi alibainisha kwamba Xiao Cui alikuwa bweha mdogo, kwa sababu mama yake aliwahi kukimbia janga nyumbani kwa wale wazee, akajigeuza kuwa binadamu ili kuwalipa wema wao.

Katika kitabu cha “Hadithi za Mashetani”, pia wako bweha wenye sura mbaya lakini roho nzuri. Hadithi ya “Bweha Mwenye Sura Mbaya” ilieleza jinsi bweha mmoja mwenye sura ya kuchukiza alivyomkuta msomi mmoja, ambaye alikuwa maskini hahehohe hata chakula kilikuwa ni shida kwake achilia mbali nguo. Bweha huyo alimsaidia maisha yake. Lakini baada ya msomi huyo kupata nguo safi, nyumba za fahari na kila kitu kwa maisha ya starehe alimwomba mchawi amfukuze bweha. Bweha alihamaki sana kutokana na msomi huyo kukosa shukrani, ndipo licha ya kurudisha yote aliyompa msomi, alimtuma shetani kumwadhibu vibaya. Kwa masimulizi ya hadithi hii mwandishi anawaonya watu wenye roho mbaya.

Katika kitabu cha “Hadithi ya Mashetani” mwandishi Pu Songling pia alitunga hadithi ya bweha kisura lakini mwenye roho katili. Hadithi ya “Kuchora Ngozi ya Mrembo” ilieleza kuwa bweha mmoja alijifunika kwa ngozi yenye sura nzuri akiishi kwa kufyonza damu za binadamu, bweha huyo mwishowe aliuawa na binadamu. Hadithi nyingine ya “Bweha Aingiaye ndani ya Jagi” ilieleza jinsi bweha mmoja mara kwa mara alivyofanya uhalifu nyumbani kwa watu, na baada ya kugunduliwa akajigeuza kuwa moshi na kujipenyeza ndani ya jagi la maua, mwenye nyumba mwerevu mara akaziba mdomo wa jagi akamwua bweha ndani.

Kwa kifupi, Pu Songling aliwaelezea wasichana wengi kwa sura ya bweha, na wasichana hao walikuwa na maadili mengi mazuri ambayo binadamu hawakuwa nayo.

“Hadithi ya Mashetani” ni maandishi makubwa katika historia ya fasihi ya Kichina, maandishi hayo pamoja na maandishi mengine yaliyoandikwa katika enzi moja yaani “Ndoto kwenye Jumba Jekundu” yaliipeleka kileleni historia ya riwaya za Kichina. Katika muda wa miaka mia mbili iliyopita kitabu hicho kimetafsiriwa kwa lugha za kigeni zaidi ya kumi na kusambazwa kote duniani. Aidha, hadithi nyingi kwenye kitabu hicho zimetengenezwa kuwa michezo ya sinema na televisheni inayowafurahisha sana watazamaji.