Hanxin Aibishwa kwa Kupita Kati ya Miguu
中国国际广播电台


       Karne ya pili K.K. ilikuwa ni Enzi ya Qin, katika enzi hiyo Ukuta Mkuu ulikuwa umeanza kujengwa. Lakini kutokana na utawala wa kikatili, enzi hiyo ilidumu kwa miaka 15 tu. mwishoni mwa enzi hiyo wakulima walifanya uasi huko na huku, wakati huo walitokea mashujaa wengi, Hanxin alikuwa mmoja kati ya mashujaa hao.

Hanxin alikuwa jemadari mkubwa, alizaliwa katika ukoo maskini, na alifiwa na wazazi wake tokea alipokuwa mtoto. Kabla ya kuwa jemadari, Hanxi alikuwa hafahamu kufanya biashara na kulima, aliishi katika hali ya umaskini kabisa na mara kwa mara alikosa chakula.

Ili aweze kuishi, ilimpasa kuvua samaki kwa mshipi kwenye mto Huaishui uliokuwa karibu na nyumbani kwake. Kulikuwa na dobi mmoja mzee, kwa kumhurumia, mara kwa mara alimpa chakula. Hanxin alisisimka sana na kumwambia mzee dobi, “Nitalipa wema wako.” Mzee dobi aliposikia hayo alikasirika na kusema, “Wewe ni mwanamume hata unashindwa kujipatia riziki. Nakupa chakula kwa kukuhurumia tu sitaki ulipe wema wangu.” Hanxin alijionea masikitiko, huku aliamua kuwa ni lazima afanye kitu.

Wenyeji walimdharau Hanxin. Siku moja kijana mmoja alitaka kumdhalilisha, alimwambia Hanxin, “Ukiwa jasiri niue kwa upanga wako, ama sivyo pita kati ya miguu yangu.” Watu wengi walikuja kutaka kuona Hanxin atakuwaje. Hanxin baada ya kufikiri alipita kati ya miguu ya huyo kijana. Watu walioshuhudia walicheka, wakiona kuwa Hanxin ni mhofu. Hii ndio “hadithi ya kumwaibisha Hanxin kwa kupita kati ya miguu”.

Hanxin alikuwa mtu mwenye mtazamo wa mbali. Alipoona kuwa jamii inapokuwa katika kipindi cha kubadilisha enzi, alijitahidi kujifunza uhodari wa kupigana vita, aliamini kuwa ataibuka katika jamii. Mwaka 209 wakulima walifanya uasi kila mahali dhidi ya utawala wa Enzi ya Qin. Hanxin alijiunga na jeshi moja, lakini hakuthaminiwa kama alivyotaka. Hatimaye alimfahamu mshauri Xiao He wa Liu Bang, wao mara kwa mara walijadiliana mambo ya kijeshi, Xiao He aliona kuwa Hanxin ni mtu hodari, kwa hiyo alijitahidi kumpendekeza Hanxin kwa Liu Bang. Lakini Liu Bang hakumthamini sana.

Siku moja Han Xin aliondoka kutoka jeshini na kukimbilia kwenyue jeshi jingine. Baada ya kusikia habari hiyo Xiao He alimkimbilia kwa farasi. Liu Bang alidhani hao wawili walitoroka. Lakini baada ya siku mbili walirudi kwa Liu Bang. Xiao He alimwambia, “Nilimkimbilia Han Xin.” Liu Bang alibabaika na kusema, “Zamani majemadari wangapi walitoroka, mbona Han Xin tu ulimkimbilia na kumrudisha?” Xiao He alisema, “Waliotoroka wote walikuwa wa kawaida, lakini Han Xin sivyo, ni mtu asiyepatikana kwa urahisi, ukitaka kupata nchi Han Xin ni mtu wa lazima.” Liu Bang alisema, “Kama ni hivyo, basi mbakize na awe jemadari mkuu.” Tokea hapo Han Xin alipomsaidia Liu Bang kuipata nchi nzima alipata ushindi mkubwa katika vita.