Hadithi ya “Kugawa Uji na Achali”
中国国际广播电台


        Fan Zhongyan alikuwa mwanasiasa na mwanafasihi mkubwa katika historia ya China, michango yake mikubwa haikuwa katika fasihi tu bali pia katika mambo ya kijeshi. Makala yake inayojulikana kama “Kumbukumbu katika matembezi ya banda la Yue Yang Lou” ni maarufu sana katika fasihi ya kale ya Kichina. Vifungu ndani ya makala hiyo “Kiongozi anapaswa awe na wasiwasi kabla ya wananchi, na afurahie matunda nyuma ya wananchi” vinasifiwa na watu kizazi hadi kizazi. Katika kipindi hiki nitawasimulieni jinsi alivyojitahidi kusoma utotoni mwake.

“Fan Zhongyan alikuwa mtu wa Enzi ya Song ya karne ya kumi. Kabla hata hajatimiza umri wa miaka mitatu alifiwa na baba yake, maisha yalikuwa ya kusikitisha sana. Alipofikisha umri wa miaka 10 aliondoka nyumbani kwenda kutafuta elimu na mwishowe alipata mwalimu katika Chuo cha Ying Tian Fu. Alipokuwa chuoni maisha yake yalikuwa ya ufukara kama maji, kwa kuwa hakuwa na fedha za kununulia chakula na kwa muda mrefu alilazimika kunywa uji tu. Kila siku asubuhi alichemsha uji na baada ya uji kupoa na kuwa mgando akaugawa pamoja na achali sehemu tatu ili asitumie zaidi sehemu moja kwa wakati mmoja.

Siku moja Fan Zhongyan alipokuwa akila, rafiki yake alikuja kumtembelea, akagundua chakula chake kilikuwa hafifu na cha kusikitisha, kwa huruma akampa fedha za kumsaidia apate chakula bora, lakini Fan Zhongyan alikataa kwa kumshukuru sana. Rafiki yake alishindwa kumshawishi, basi siku ya pili akamletea chakula kizuri cha kufisha ubuge. Fan Zhongyan alilazimika kukipokea.

Siku kadhaa zilipita, rafiki yake huyo alikuja tena kumtembelea, akagundua kwamba chakula alichomnunulia hakikuguswa hata kidigo, akakasirika na kusema, “Wewe unajiheshimu kupita kiasi, hata unakataa chochote cha wengine.”

Fan Zhongyan alitabasamu na kusema, “Ndugu, umenielewa vibaya. Sio mimi nakataa chakula kitamu, bali sithubutu kukitumia. Kwani nikila chakula kinono kama hiki cha nyama na samaki, nitashindwa kumeza uji na achali baadaye. Wema wako naupokea, halahala usinihamakie.” Kusikia hayo rafiki yake akamheshimu zaidi.

Fan Zhongyan aliwahi kuulizwa na wengine malengo yake katika maisha yake. Alijibu, “Malengo yangu ni kuwa daktari hodari au waziri mkuu mwema, kwani daktari anawaokoa wagonjwa, na waziri mkuu anaiendesha dola.” Na kweli baadaye alikuwa waziri mkuu akawa mwanasiasa mashuhuri katika historia ya China.

Fan Zhongyan, kwa upande mmoja alistawisha elimu na kwa upande mwingine alifanya mageuzi ya idara za serikali iliyokuwa ya umangi meza. Alijenga shule nyingi kote nchini na kuongeza walimu ili kuwalea watu hodari wanaohitajika sana katika ujenzi wa taifa. Na yeye mwenyewe aliwathamini kwa vitendo watu wenye umahiri wa fani mbalimbali, mwanasiasa Ou Yangxiu, mwanafasihi Zhou Dunyi na mwanafasafa Zhang Zai n.k, wote walipata kusaidiwa naye.

Fan Zhongyan mbali ya kushughulika na mambo yake ya taifa naye pia alijinyima wakati kuandika maandishi mengi mazuri. Ni stahili yake kusifiwa kwamba yeye alipinga tungo za kuchezea maneno tu bila maudhui. Alitetea fasihi ifungamane na hali ilivyo ya jamii ili kupeleka mbele jamii na maendeleo ya binadamu. Utetezi huu ulikuwa umeathiri sana maendeleo ya fasihi ya baadaye.